19/08/2013
LEO NAASI POMBE_21 JULAI 2013.
Ni mengi nimeshaona, leo hii kuamua, pombe siitaki tena, wenzangu nisikizeni,
Wazazi wameshanena, mvinyo kuondokea, leo hii ninakana, nawasihi nipateni,
Vigumu haya kuona, jaribu kufikiria, hu’tojua hata kona, kuanguka matopeni,
K**a tawi kwenye shina, hutoweza achilia, mengi kwangu kuyabana, kupotezea mapeni,
Nilianza kwa kuonja, ndo’ shida kujitakia, nisiweze kufahamu, ni shimo kujichimbia,
Kapatana na wanjanja, sungura hato’fikia, onja upate utamu, ushauri kuufwata,
Pole pole k**a panja, upeo nikafikia, moja mbili kila zamu, chupa kuzifungulia,
Wala Dada sio wanja, urembo kujipakia, punde kapata wazimu, chakari kupindukia,
Baadaye ‘kawa sugu, wenzangu kuwazomea, njia zote kuzijua, sikutaka la mwadhini,
Nikazidi kuwa pwagu, kipitacho kumezea, gizani hata kwa jua, ‘kuhepa’ msikitini,
Chakula kikawa njugu, pombe kuteremushia, haya yote sikujua, kulala miferejini,
Kupitia kwenye gugu, soni nimeshajitia, lilobaki nilojua, ni ulevi vijijini,
Sikufika maskani, nifikapo ni bahati, kurauka ni dosari, Afisini kuchelewa,
Maruwe ruwe kichwani, kuchanika langu shati, kusiwe lolote shwari, umeachwa kwa ukiwa,
Siendi tena pombeni, nishasema hunipati, mvinyo basi kwaheri, kulewa sio kipawa,
Nipitapo mitaani, langu jina mada nyeti, wala kusiwe na siri, yaso kweli kunenewa,
‘batili hisia zako, na chafu ikawa safi, wabaya huwa warembo, kila bovu huwa zuri,
Wangu atakuwa wako, utadhani huyu hafi, utasifu liso pambo, hutaki hata habari,
,sitambue ulioko, ovyo kuzabwa makofi, sababu ikiwa tembo, maisha kuyajasiri,
Nimeonya tena siko, nimekiri kwake wifi, mfano bora wa tambo, kaka hima jinawiri,
Kahofu uhai wangu, kupokonywa kila mara, nikaporwa yangu mali, kukawa sintofahamu,
Naondoka kwenye wingu, uwamuzi wa imara, nikamusihi jalali, mola bora nirehemu,
Kwako ninatoa fungu, ninatoa na kafara, niepushe hii hali, amani kwangu idumu,
Kaka njoo wanguwangu, tuepuke ufukara, karibuni tujadili, tuepukeni hukumu.