21/04/2026
ZEEA YAKUTANA NA BALOZI WA ITALIA NCHI TANZANIA, YALENGA KUWAPATIA WAJASIRIAMALI FURSA ZA KIMATAIFA
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), ndugu Juma Burhan Mohamed, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Balozi Giuseppe Sean Coppola, kwa lengo la kutafuta na kufungua fursa za kiuchumi, zitakazowawezesha wajasiriamali wa Zanzibar kukuza biashara zao na kuongeza ushindani katika soko la ndani na kimataifa.
Mkurugenzi huyo amemueleza Balozi Coppola jinsi ZEEA inavyotekeleza majukumu yake katika kuwawezesha wajasiriamali, ikiwemo utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali, uwezeshaji wa mitaji, pamoja na kusaidia upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zao, ili kuongeza tija, kukuza biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi jumuishi.
Katika kuendana na mabadiliko ya kasi ya ukuaji wa teknolojia, Mkurugenzi Juma amesisitiza kuwa ZEEA inahitaji kushirikiana na washirika wa maendeleo watakaosaidia kuwajengea uwezo wajasiriamali katika matumizi ya teknolojia za kisasa, ili kukuza uzalishaji wa bidhaa na huduma, sambamba na kuongeza ishandani katika upatikanaji wa masoko.
Naye Balozi Coppola ameeleza kuwa Serikali ya Italia inaandaa maonesho, programu na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazolenga kuwajengea uwezo wajasiriamali katika nyanja tofauti, ikiwemo kilimo, utalii na uchumi wa buluu, pamoja na sekta nyingine zenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Aidha, ameishauri ZEEA kuandaa wasilisho rasmi litakaloeleza kwa kina shughuli na mipango ya taasisi hiyo, ili kubainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano na namna ambavyo Serikali ya Italia na taasisi zake zinaweza kushirikiana na ZEEA katika kuwawezesha wajasiriamali kwa ufanisi zaidi.