16/07/2026
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Jullieth Magandi, amefungua mafunzo ya Usimamizi wa Fedha na Uwajibikaji (Financial Management and Stewardship Workshop) leo, Julai 9, katika Hoteli ya Golden Tulip, yakilenga kuimarisha uelewa wa viongozi wa ngazi mbalimbali hospitalini hapo kuhusu usimamizi bora wa fedha na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja, Dkt. Magandi amesema kuwa usimamizi wa fedha na uwajibikaji ni muhimu kwa kila kiongozi, na kuongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kusimamia rasilimali kwa ufanisi na kufanya maamuzi sahihi yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma.
“Usimamizi wa fedha si jukumu la wataalamu wa fedha pekee. Kila kiongozi anayesimamia rasilimali ana wajibu wa kuhakikisha fedha zinatumika kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji. Nawasihi mtumie mafunzo haya k**a fursa ya kuongeza maarifa, kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo utakaowawezesha kutekeleza majukumu yenu kwa weledi zaidi,” amesema Dkt. Magandi.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wakurugenzi, wakuu wa idara na vitengo, pamoja na wasimamizi wa uendeshaji wa vitengo mbalimbali (Business Managers), ambapo wanapata uelewa kuhusu misingi ya usimamizi wa fedha, matumizi sahihi ya rasilimali na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu.