14/07/2026
SERIKALI YAHAKIKISHA KUENDELEA KUZIWEZESHA TIMU ZA TAIFA KUFANYA VIZURI KIMATAIFA
Serikali imeahidi kuendelea kuziwezesha timu za taifa zinazoshiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa ili kuhakikisha zinafanya vizuri na kuiletea Tanzania heshima.
Kauli hiyo ilitolewa Julai 13, 2026, na Afisa wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Oscar Zabron, wakati alipoitembelea Timu ya Taifa ya Judo kambini Ukonga, jijini Dar es Salaam, inayojiandaa kushiriki Mashindano ya Jumuiya ya Madola.
Oscar amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila timu ya taifa inayoshiriki mashindano ya kimataifa inapata maandalizi bora na mazingira wezeshi ya kufanya vizuri.
Aidha, amewahimiza wachezaji kuitumia kikamilifu kambi ya maandalizi kwa kufanya mazoezi kwa bidii na kuzingatia maelekezo ya makocha, akisisitiza kuwa ushindi watakaoupata utakuwa ni fahari ya Watanzania wote.
"Serikali itaendelea kuziwezesha timu za taifa ili zifanye vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Tunawaomba muweke nguvu katika mazoezi na kufuata maelekezo ya makocha, kwani ushindi mtakaoupata ni wa Watanzania wote," amesema Oscar.
Timu ya Taifa ya Judo inaendelea na maandalizi ya mwisho ikiwa na matumaini ya kuiwakilisha vyema Tanzania na kuwania medali katika Mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Glascow, Scotland.
Kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Serikali imeratibu na kugharamia mahitaji muhimu ya kambi, ikiwemo malazi, chakula na posho kwa wachezaji, ili kuwawezesha kufanya maandalizi katika mazingira bora kuelekea mashindano hayo.
1m