08/08/2026
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemus Mk**a, akizungumnza katika hafla ya uzinduzi wa Kielelezo cha Viwango vya Faida vya Dhamana za Serikali (Government Securities Yield Curve), iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Amesema masoko ya fedha nchini yameendelea kukua, huku thamani ya uwekezaji katika masoko hayo kwa ujumla ikiongezeka kwa asilimia 45.Ukuaji huo umeonekana katika maeneo mbalimbali ya soko, ambapo soko la hisa la Dar es Salaam limeongezeka kwa asilimia 79, uwekezaji katika hati fungani za Serikali na taasisi ukikua kwa asilimia 48, huku mifuko ya uwekezaji wa pamoja ikiongezeka kwa asilimia 79.
Mk**a amesema uzinduzi wa kielelezo hicho ni hatua nyingine ya kuongeza uwazi katika masoko ya fedha, kwa kuwapatia wawekezaji taarifa za bei elekezi zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi na kuongeza ufanisi katika shughuli za uwekezaji.
Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, amesema soko imara la fedha ni muhimu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa, huku akisisitiza umuhimu wa upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati kwa washiriki wa soko.
Amesema kielelezo hicho kitasaidia kuongeza ufanisi wa miamala katika soko la fedha, kuboresha huduma na kuwawezesha wawekezaji kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa sahihi.