22/06/2026
MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MIKOPO YA 10% YAANZA DODOMA, RC SENYAMULE ASISITIZA UREJESHAJI NA TIJA
Na Mwandishi Wetu ,
DODOMA RS
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, tarehe 22 Juni 2026 amefungua rasmi mafunzo ya usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye mahitaji maalumu yanayofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dodoma.
Akifungua mafunzo hayo, Mhe. Senyamule alisisitiza umuhimu wa usimamizi bora wa mikopo hiyo ili kuongeza tija kwa walengwa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Alisema mafunzo hayo yanakuja wakati Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiendelea kuimarisha utoaji wa mikopo kwa makundi maalumu.
Alieleza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo maafisa wa Halmashauri katika tathmini ya wakopaji, usimamizi wa mikopo, mikakati ya urejeshaji na matumizi ya mifumo ya kidijitali. Pia aliwataka viongozi na watendaji kuzingatia uwazi, haki na nidhamu katika usimamizi wa mikopo hiyo, huku akiwahimiza wanufaika kurejesha mikopo kwa wakati ili mfuko huo uwe endelevu.
“Mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo maafisa wa Halmashauri wanaohusika na usimamizi wa mikopo hiyo katika maeneo ya tathmini ya uwezo wa wakopaji, usimamizi wa hatari za mikopo, mikakati ya urejeshaji wa mikopo pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali” - Amesema Senyamule.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliipongeza CBE kwa mafanikio yake ya kitaaluma, ikiwemo kushika nafasi ya 10 miongoni mwa vyuo vya elimu ya juu Nchini, na kuitaka kuendelea kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha utoaji na usimamizi wa mikopo ya asilimia 10.
Kwa upande wake, Mkuu wa CBE Kampasi ya Dodoma, Prof. Edda Tandi Lwoga, alisema chuo hicho kinaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali bila ada kwa wanawake, vijana na wajasiriamali wadogo, ambapo katika kipindi cha miaka mitano, jumla ya wajasiriamali 4,500 wamepatiwa mafunzo, pamoja na wahudumu wa mabasi 2,418 na mawakala wa mali zisizohamishika 45.
Prof. Lwoga pia aliwapongeza Wakurugenzi wa Halmashauri za Lindi, Babati na Karatu kwa kutenga bajeti na kuwawezesha Maafisa wao kushiriki mafunzo hayo, akiwahimiza kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu.
Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia Juni 22 hadi 25, 2026 yakiwashirikisha maafisa kutoka Halmashauri mbalimbali, ikiwemo Babati na Karatu.