Wizara ya Fedha

Wizara ya Fedha Ukurasa Rasmi wa Wizara ya Fedha Tanzania.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (MB), ameshiriki katika Kilele cha Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festiv...
14/08/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (MB), ameshiriki katika Kilele cha Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival) lililohitimishwa leo, tarehe 14 Agosti 2026, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Tamasha hilo lililofana sana linaakisi umuhimu wa kuendeleza tamaduni, sanaa na urithi wa Zanzibar, pamoja na kutumia matamasha k**a fursa ya kuimarisha mshik**ano, kukuza utalii na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

Miongoni mwa matukio aliyofanya Mhe. Balozi Omar katika Tamasha hilo ni kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya TRA, Kizimkazi, Zanzibar, litakalokuwa na ghorofa moja, ambapo hadi kukamilika kwake linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 3.6.

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani zimeanza mazungumzo ya pande mbili kwa lengo la k...
14/08/2026

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani zimeanza mazungumzo ya pande mbili kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, hususan katika miradi yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi na Uchumi wa Taifa.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Fedha Mtumba, jijini Dodoma, yalijikita katika maeneo mbalimbali ya kimkakati, yakiwemo maji na usafi wa mazingira, afya, nishati, matumizi endelevu ya rasilimali za asili na uhifadhi wa mazingira, upatikanaji wa haki, usimamizi bora wa fedha za umma pamoja na usawa wa kijinsia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa Pande Mbili, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alisema mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Ujerumani, ambao una historia ya zaidi ya miongo sita.

Alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani ulianza tangu miaka ya 1960, ambapo waasisi wa mataifa hayo waliweka misingi ya uhusiano na ushirikiano ambao umeendelea hadi sasa na mwaka 1975 Tanzania na Ujerumani zilisaini Mkataba wa Mfumo wa Ushirikiano (Framework Agreement) ulioweka misingi ya namna ushirikiano kati ya pande hizo mbili utakavyoendelezwa.

“Ujerumani imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Tanzania katika sekta mbalimbali, zikiwemo maji, mawasiliano, utalii, maendeleo ya watu na ustawi wa jamii” Alisema Bw. Mwandumbya

Alisema kuwa majadiliano hayo yatawezesha wataalamu kutoka pande zote mbili kutathmini na kuweka vipaumbele vya miradi na maeneo ya ushirikiano yatakayotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Aliongeza kuwa baada ya timu za wataalamu kukamilisha majadiliano na kufikia makubaliano, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani zinatarajiwa kuchukua hatua zinazofuata za kurasimisha makubaliano hayo, ikiwemo kusaini mkataba wa ushirikiano wa maendeleo na pia kuendekeza mazungunzo hayo mwezi Novemba 2026.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, alisema Tanzania iko tayari kuimarisha na kuhuisha ushirikiano wake wa muda mrefu na Ujerumani ili kuendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Alisema Dira 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kipato cha kati cha juu, mseto, himilivu na jumuishi, huku ikihakikisha wananchi wanapata maisha bora na ustawi wa hali ya juu.

“Tanzania imejiwekea lengo la kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 na kuongeza pato la Taifa kwa mtu mmoja hadi takribani dola 7,000, kutoka uchumi wa sasa unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 90”, alisema Dkt. Kida.

Aliongeza kuwa pamoja na hayo, nchi inalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa umaskini, kuondokana na umaskini uliokithiri na kukabiliana na umaskini wa chakula, sambamba na matumizi endelevu ya rasilimali na ulinzi wa mazingira na kwamba ushirikiano wa nchi hizo mbili utachangia kufikia malengo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani, Bw. Joachim Schmitt, alisema Serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania huku akibainisha mkakati mpya wa ushirikiano ambao utaelekezwa katika maeneo yenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa, huku ikisisitiza umuhimu wa kulinda utawala wa sheria, nafasi ya asasi za kiraia, amani na usalama.

Alisema Ujerumani inataka ushirikiano huo uwe wa kimkakati zaidi na uendane na vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania, badala ya kutegemea miradi midogo isiyounganishwa katika mwelekeo mpana wa maendeleo.

Bw. Schmitt, alisema Ujerumani imeweka msisitizo maalumu katika ushirikiano wa kiuchumi, maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji, ikilenga kuwashirikisha zaidi kampuni za Ujerumani na Tanzania katika miradi ya maendeleo.

Mkutano wa Mazungumzo hayo ya siku mbili, yamewakutanisha wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiongozwa na taasisi na wizara mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Katiba na Sheria, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Na kwa upande wa Ujerumani umewakilishwa na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani pamoja na taasisi zake za ushirikiano wa maendeleo, zikiwemo KfW na GIZ.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), ameimwagia sifa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kwa utendaji uliotuk...
13/08/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), ameimwagia sifa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kwa utendaji uliotukuka uliowezesha Mamlaka hiyo kuendelea kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kila mwezi na kueleza imani yake kwamba kwa kushirikiana na walipakodi, wataweza kuvuka lengo walilopangiwa la kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 42 katika Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Mhe. Balozi Omar, ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya TRA, Kizimkazi, Zanzibar, litakalokuwa na ghorofa moja, ambapo hadi kukamilika kwake linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 3.6.

Sifa hizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, zinafuatia maelezo ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Bw. Yusuph Mwenda ambapo alisema katika mwezi Julai mwaka huu, Mamlaka yake imevuka malengo kwa kukusanya shilingi trilioni 3.2 ikilinganishwa na malengo waliyopangiwa ya kukusanya shilingi trilioni 2.

Alisema kuwa mafanikio ya TRA katika ukusanyaji wa mapato yanatokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, Bunge na wadau wa kodi, ambapo mwezi Julai pekee, Mamlaka ilikusanya zaidi ya Shilingi trilioni 3.245 ikilinganishwa na lengo la mwezi la kukusanya shilingi trilioni 2.971, sawa na ufanisi wa asilimia 109 ya lengo, na ukuaji wa asilimia 21.

“Kutokana na usimamizi wako mzuri Mhe. Waziri wa Fedha, na ushirikiano na walipakodi, tunakuhakikishia tutavuka lengo hilo na kupita, ishara inayoonesha kwamba tumeanza mwaka wa fedha kwa nguvu kubwa, na tuna imani tutafikia na kuvuka malengo tuliyowekewa” alisema Bw. Mwenda.

Aidha, CPA Mwenda alisema kuwa katika kipindi hicho cha Julai, 2026, TRA imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 325, fedha mabazo ni asilimia 70 ya makusanyo yote na kuzipeleka moja kwa moja kwenye Mifuko 11 ya ujenzi wa miundombinu katika sekta mbalimbali zikiwemo Barabara, maji, utalii na sekta nyingne.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa Ofisi za TRA, Kizimkazi-Unguja Zanzibar inayojengwa na Kampuni ya CRJE ya China, ni sehemu ya ujenzi wa Ofisi k**a hizo 49 zinazojengwa nchi nzima zikitarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 32 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ulipaji kodi na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb) aliwahakikishia watanzania kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inajitegemea kwa kutumia mapato yake ya ndani kutekeleza miradi yake ya maendeleo ambapo katika Mwaka wa Fedha 2026/2027, imepanga kujitegemea kwa zaidi ya asilimia 74.

Alisema kuwa ujenzi wa Ofisi za TRA Kizimkazi na maeneo mengine nchini, ni mikakati ya Serikali ya kuimarisha huduma, kurahisisha shughuli za biashara, kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuwawezesha watumishi kufanya kazi katika mazingira bora kwa ajili ya kuongeza mapato yanayowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, nishati, maji, kuimarisha huduma za afya na kuwekeza katika elimu.

Mhe. Balozi Omar ameuagiza Uongozi wa TRA kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA kutumia miundombinu ya Ofisi hizo na nyingine zitakazo jengwa Visiwani Zanzibar, ili wadau wa kodi wapate huduma kikamilifu, jambo ambalo Kamishna wa TRA Bw. Mwenda aliahidi kulifanyia kazi.

Aidha aliwataka wafanyabiashara na wananchi kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati, kwa ukamilifu na kwa hiari, akisisitiza kuwa ulipaji wa kodi unapaswa kuwa jambo la fahari kwa kila mwananchi anayewajibika na Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara katika kuboresha huduma za kodi na kupunguza changamoto zinazowakabili, huku ikitarajia wafanyabiashara nao kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini, Mhe. Othman Ali Maulid, alitoa wito kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi na kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa wananchi, lakini pia kusikiliza changamoto za wananchi na wafanyabiashara.

Akiongea kwa niaba ya Wafanyabishara wa sekta ya hoteli na utalii Zanzibar, Bw. Henry Kaunda, aliishukuru TRA na ZRA kwa kushirikina na wafanyabiashara na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili hatua iliyochangia ulipaji kodi kwa hiari na kuomba elimu zaidi ya mlipakodi iendelee kutolewa kwa wafanyabiashara.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesema Mkoa wa Mbeya na maeneo ya Nyanda za Juu Kusini yana fursa ...
12/08/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesema Mkoa wa Mbeya na maeneo ya Nyanda za Juu Kusini yana fursa kubwa ya kuongeza mchango wake katika uchumi wa Tanzania kwa kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kukuza shughuli za viwanda.

Mhe. Balozi Omar amesema hayo alipokuwa akizungumza wakati alipotembelea Ofisi za Mkoa za Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Mbeya, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo.

Alieleza kuwa eneo la Nyanda za Juu Kusini linachukua takribani asilimia 20 ya eneo lote la Tanzania, lakini mchango wake katika pato la Taifa bado haujaendana kikamilifu na ukubwa wa eneo na fursa zilizopo.

Mhe. Balozi Omar alisema hali hiyo inaonesha kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, madini, viwanda na sekta nyingine za uzalishaji ili Mkoa wa Mbeya na Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla uwe na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa.

“Bado tuna fursa kubwa sana ya kuimarisha mchango wetu katika pato la Taifa uendane na eneo tulilonalo, na si kwa sababu hatuna fursa,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, katika kusisitiza uchakataji wa mazao, alisema kuwa Serikali itaendela kuweka mkazo mkubwa katika kuongeza thamani ya mazao ndani ya nchi ili nchi iondokane na mfumo wa kuzalisha mazao na kuyauza bila kuyachakata, hatua ambayo itasaidia kuongeza ajira, mapato kwa wananchi na mapato ya Serikali, huku ikiiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na mnyororo mzima wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Msisitizo wetu uwe kwenye mnyororo wa thamani, Tunaweza kulima, kuvuna na kuuza mazao, lakini tunahitaji kuwa sehemu kubwa zaidi ya mnyororo wa thamani kwa kuhakikisha uchakataji unafanyika hapa nchini,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Alisema badala ya Tanzania kubaki katika hatua za awali za uzalishaji na kuuza malighafi, ni muhimu kuongeza uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ili bidhaa zinazotokana na rasilimali za Tanzania ziweze kuzalishwa nchini na kuuzwa katika masoko ya ndani na nje na hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira, mapato ya wananchi na Serikali, pamoja na kuchochea ukuaji wa viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Akizungumzia shughuli za uchimbaji wa madini mkoani Mbeya, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa mazingira na afya za wachimbaji pamoja na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka shughuli za uchimbaji, kwa kuwa pamoja na manufaa ya kiuchumi yanayotokana na uchimbaji wa madini, Serikali inapaswa kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia usalama wa afya za watu na mazingira.

Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika Wilayani Chunya, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Serikali itafanya jitihada ya kuboresha miundombinu ya umeme utakaowezesha uchimbaji na uzalishaji wa dhahabu ufanyike kwa ufanisi na kuongeza tija kwa wananchi na mapato ya Serikali kwa ujumla.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, alisema Mkoa huo una uwezo mkubwa wa kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa kupitia sekta za uzalishaji, hususan kilimo, viwanda na biashara.

Mhe. Mwalunenge alisema kuwa Mbeya inaendelea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya uzalishaji wa mazao ya biashara k**a chai, kahawa na kakao, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mazingira yatakayowezesha wakulima kupata masoko ya uhakika pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao hayo.

“Nasisitiza Serikali ione umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya biashara na viwanda, ikiwemo ujenzi wa bandari kavu na kongani za viwanda, ili kuifanya Mbeya kuwa kitovu cha biashara na uzalishaji kwa Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani, kwa kuwa nafasi ya kijiografia ya Mbeya, pamoja na uzalishaji mkubwa wa kilimo katika Nyanda za Juu Kusini, inatoa fursa ya kuunganisha uzalishaji, uchakataji na masoko ya ndani na nje ya nchi” aliongeza Mhe. Mwalunenge.

Naye Mbunge wa Jimbo la Lupa-Chunya, Mhe. Masache Kasaka, alisema utekelezaji wa miradi ya maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa wakati ni muhimu katika kuongeza kasi ya shughuli za uzalishaji na kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Mbeya.

Mhe. Kasaka alisema Chunya ina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa kupitia uzalishaji wa dhahabu na tumbaku, huku akieleza kuwa wilaya hiyo inaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu miongoni mwa wachimbaji wadogo nchini, ikizalisha wastani wa kilo 400 kwa mwezi ambapo k**a Serikali itaboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya uzalishaji kutasaidia kuongeza uzalishaji wa dhahabu na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi.

“Chunya ina fursa kubwa katika uzalishaji wa tumbaku, ambapo licha ya kilimo hicho kufanyika katika eneo dogo ukilinganisha na mikoa mingine, wilaya yetu imeendelea kuwa miongoni mwa wazalishaji muhimu na k**a kutaimarishwa kwa miundombinu ya umeme, maji na barabara, pamoja na kukamilishwa kwa miradi inayotekelezwa, kutasaidia wananchi kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika sekta za uzalishaji” alisema Mhe. Kasaka.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, ameongoza Ujumbe w...
11/08/2026

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, ameongoza Ujumbe wa Serikali ya Tanzania kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, katika kikao na Ujumbe wa Benki ya Dunia kilicholenga kuhitimisha maandalizi ya kitaalamu ya Programu ya Uendelezaji wa Ushoroba wa Kati wa Maendeleo ya Kiuchumi Utakaoongeza Ajira kwa Vijana (CATALYZING JOBS AND RESILIENT GROWTH IN THE CENTRAL CORRIDOR MULTIPHASE PROGRAMMATIC APPROACH
(KAZI MPA).

Kikao hicho kilifanyika kwa lengo la kuwasilisha na kujadili matokeo ya maandalizi yaliyofanywa kwa pamoja kati ya Serikali na Benki ya Dunia, pamoja na kukubaliana hatua zinazofuata kuelekea kukamilisha maandalizi ya Programu hiyo, kilichofanyika, Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Katika kikao hicho, pande hizo zilijadili kwa kina maeneo muhimu ya utekelezaji wa KAZI MPA, huku zikisisitiza umuhimu wa programu hiyo katika kuchochea mageuzi ya kiuchumi, kuongeza uwekezaji na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Aidha, KAZI MPA inalenga kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana, pamoja na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa kupitia kuendeleza miundombinu na mazingira wezeshi ya shughuli za kiuchumi katika Ushoroba wa Kati.

Utekelezaji wa programu hiyo unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya jitihada za Serikali katika kutafsiri kwa vitendo malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hususan katika kujenga uchumi wenye tija, jumuishi na stahimilivu, unaotoa fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na biashara.

Ujumbe wa Serikali katika kikao hicho uliwahusisha pia Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Adolf Ndunguru, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvivu Bi. Agness Meena, Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Nsubil Joshua, Naibu Makatibu Wakuu Wizara ya Kilimo, Prof. Peter Msoffe na Mhandisi Athumani Kilundumya pamoja na Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango Bw. Sosthenes Kewe.

Kwa upande wa Ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Meneja wa Benki ya Dunia, Kitengo cha Utekelezaji wa Sekta ya Usafiri, Afrika Mashariki na Kusini, (Practice Manager for Transport in Eastern and Southern Africa), Bw. Binyam Reja.

Kikao hicho ni hatua muhimu kuelekea kukamilisha maandalizi ya KAZI MPA na kuweka msingi wa utekelezaji wa programu inayolenga kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika uchumi wa kikanda na kimataifa.

Tanzania na Marekani zimeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika sekta mbalimbali zikiw...
11/08/2026

Tanzania na Marekani zimeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika sekta mbalimbali zikiwemo madini adimu, nishati, afya, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi, pamoja na dhamira ya kuendeleza mazungumzo na ushirikiano wa kitaalamu kwa manufaa ya nchi hizo mbili.

Hayo yameafikiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb) na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Andrew Lentz, walipokutana na kufanya mazungumzo ya katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo pia walieleza umuhimu wa kuendelea kutumia majadiliano ya kitaalamu na ushirikiano wa Serikali kwa Serikali katika kushughulikia maeneo yenye umuhimu wa kimkakati, ikiwemo maendeleo ya sekta ya Nishati ya Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas (LNG).

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Andrew Lentz, alisisitiza kuwa mawasiliano ya karibu na ushirikiano kati ya wataalamu wa pande zote ni muhimu katika kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

Aidha, walijadili fursa za kuendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini, ikiwemo miradi mikubwa ya madini na kuongeza thamani ya rasilimali nchini, ambapo walikubaliana kuhusu umuhimu wa kuwa na uratibu mzuri wa Serikali na wawekezaji ili kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa kwa ufanisi na kutoa manufaa kwa uchumi na wananchi.

Kwa upande wa afya, alisema kuwa hivi karibuni, Marekani na Tanzaniaa zimesaini makubaliano ya kuendeleza sekta ya afya yatakayogharimu dola za Marekani bilioni 3.1 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya afya, kukabiliana na magonjwa mbalimbali na kujenga uwezo wa ndani, kuelekea kwenye mifumo endelevu ya afya inayoongeza uwezo wa Tanzania kugharamia na kusimamia huduma za afya kwa muda mrefu, sambamba na kuimarisha uwezo wa kitaifa katika kinga, ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa.

“Tunatambua umuhimu wa uwekezaji katika miundombinu ya afya, uzalishaji wa bidhaa za afya nchini na kuimarisha taasisi zinazohusika na afya ya umma na Ushirikiano huu unalenga kuongeza uwezo wa Tanzania kukabiliana na changamoto za kiafya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na endelevu” alisema Mhe. Balozi Lentz

Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), alisema kuwa kuna nafasi kubwa ya kubadilishana uzoefu kuhusu namna Serikali hizo zinavyoweza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kifedha na kitaalamu, na Serikali inatambua juhudi zinazoendelea za wataalamu wa pande zote mbili katika kuimarisha mifumo ya kifedha, ikiwemo maendeleo ya soko la dhamana za Serikali, ambazo zinatajwa k**a mfano wa ushirikiano wa kitaalamu unaoweza kutoa manufaa ya muda mrefu kwa uchumi wa Tanzania.

“Kwa ujumla, mkutano huu umeonesha dhamira ya Tanzania na Marekani ya kuendeleza ushirikiano wa karibu katika maeneo ya kimkakati, na msisitizo mkubwa ukiwa katika kuimarisha uwekezaji, kujenga uwezo wa ndani, kuongeza thamani ya rasilimali na kuhakikisha ushirikiano huo unaleta matokeo chanya na endelevu kwa wananchi” alisema Mhe. Balozi Omar.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria Wizara ya Fedha, Bi. Mwantumu Sultan, Mshauri wa Siasa na Uchumi Ubalozi wa Marekani Nchini, Bi. Rebecca Hunter, na wataalamu wengine wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Serikali imesema uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika na kwamba uwekezaji katika sekta mbalimbali, hususani madini, g...
11/08/2026

Serikali imesema uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika na kwamba uwekezaji katika sekta mbalimbali, hususani madini, gesi, nishati, kilimo na miundombinu, unatarajiwa kutoa msukumo mkubwa kwa ukuaji wa uchumi.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), wakati akifungua mkutano na wataalamu wa Kampuni ya Kimataifa ya Tathmini ya Madeni ya (Fitch Ratings), uliofanyika kwa njia ya mtandao, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kufanya mapitio ya hali ya uchumi wa Tanzania.

Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Mageuzi ya Kodi iliyoundwa na Serikali, jambo ambalo limeendelea kukuza uchumi wa nchi.

‘’Upande wa ukuaji wa uchumi tumetoka asilimia 5, mwaka mwaka 2024, tumekwenda asilimia 5.9 mwaka jana, mwaka huu tunategemea uchumi utakuwa kwa asilimia 6.3 hatujafikia viwango ambavyo vilikuwa kabla ya COVID 19 lakini tunaendelea vizuri’’ alisema Mhe. Balozi Omar.

Alisema kuwa, moja ya maeneo muhimu yaliyojadiliwa na Fitch ni maendeleo makubwa yanayoendelea katika sekta ya madini na uchakataji wa madini, huku akieleza kuwa Tanzania ina miradi mikubwa ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi na ikitekelezwa itakuwa na mchango mkubwa katika uchumi.

‘’Kuna miradi mingine mikubwa ukiwemo wa Nyanzaga wa uchimbaji wa dhahabu Mwanza ambao unatarajiwa kuwekeza zaidi ya dola milioni 500, kuna miradi mingine ambayo inaendelea upande wa aluminiam – Songea, Chuma- Liganga, Chuma -Dodoma, na miradi mingine kwa hiyo kwa ujumla kwenye sekta hii kuna uwekezaji mkubwa ambao unatarajiwa kuleta msukumo mkubwa katika uchumi wetu’’ Alisema Mhe. Balozi Omar (Mb).

Aliongeza kuwa kwa ujumla sekta ya madini inaendelea kuwa na nafasi kubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi, hasa kutokana na ongezeko la uwekezaji unaotarajiwa katika uchimbaji na uchakataji wa madini hapa nchini.

Alisema Mradi mkubwa wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG), ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuleta msukumo mkubwa katika uchumi, pamoja na mradi wa madini ya niobium ambao tayari umesainiwa na unatarajiwa kuvutia uwekezaji wa takribani dola milioni 442.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza athari za mabadiliko ya bei za mafuta na bidhaa nyingine muhimu kwa kutumia sera na mifumo mbalimbali ya kiuchumi.

Kwa upande wa Fitch, majadiliano yaliongozwa na mchambuzi Mkuu anayeshughulikia Tanzania, Bw. José Mantero, ambapo majadiliano hayo yalilenga kuwapa wachambuzi hao fursa ya kupata taarifa za kina kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania, utekelezaji wa sera za kibajeti na fedha, pamoja na mikakati ya Serikali katika usimamizi wa deni la Taifa.

Aidha, wachambuzi hao walijikita katika kutathmini athari za vita kati ya Iran katika uchumi wa Tanzania, hususan mwenendo wa bei za mafuta na mbolea, pamoja na hatua na mikakati inayochukuliwa na Serikali kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, Kamishna Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa, Nuru Ndile, kwa njia ya mtandao.

Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani Ocean Road imeanza kutekeleza zoezi la utoaji wa elimu kuhusu sa...
10/08/2026

Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani Ocean Road imeanza kutekeleza zoezi la utoaji wa elimu kuhusu saratani pamoja na vipimo vya uchunguzi wa awali wa saratani kwa watumishi wa Wizara hiyo ili kuongeza uelewa wa namna ya kujikinga, kutambua dalili za awali na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na ugonjwa huo.

Zoezi hilo litakalohusisha utoaji wa elimu kuhusu saratani mbalimbali, ikiwemo saratani ya matiti, tezi dume na shingo ya kizazi, pamoja na vipimo vya awali linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 10 hadi 14 Agosti 2026, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Mtumba, jijini Dodoma.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, alisema ni muhimu kwa watumishi kufuatilia elimu ya afya ya saratani ili kuwa na uelewa wa kutosha kukabiliana na ugonjwa huo.

‘‘Ni muhimu kuwa na uelewa sahihi kuhusu saratani, hususan kwa kuzingatia kwamba utambuzi wa ugonjwa huo katika hatua za awali una nafasi kubwa katika matibabu na kuokoa maisha’’’ Alisema Bw. Sendo.

Aliwasisitiza watumishi wa Wizara hiyo kutumia fursa hiyo kupata elimu pamoja na kufanya vipimo vya awali vinavyotolewa ili kufahamu hali zao za afya.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Saratani, Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Frank Ruta, aliwahimiza watumishi hao kutopuuza mabadiliko au dalili zisizo za kawaida katika miili yao na kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na ushauri wa kitaalamu.

Alisema utambuzi wa saratani katika hatua za awali unaongeza nafasi ya mafanikio ya matibabu, hivyo jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuchukua hatua za mapema katika kuzuia na kukabiliana na saratani.

Dkt. Ruta alisemna elimu hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uelewa wa watumishi na jamii kwa ujumla kuhusu afya na kuwahamasisha kuchukua hatua za mapema katika kuzuia na kukabiliana na saratani.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya bajeti na usimamiz...
10/08/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya bajeti na usimamizi wa fedha za umma kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, hatua inayolenga kuhakikisha rasilimali za Serikali zinatumika kwa ufanisi katika kuchochea maendeleo jumuishi.

Mhe. Balozi Omar (Mb), aliyasema hayo jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, katika Ukumbi wa Mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square jijini Dodoma.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Wizara ya Fedha na UN Women, hususani katika utekelezaji wa Bajeti inayozingatia Masuala ya Kijinsia (Gender-Responsive Budgeting – GRB).

‘’Serikali ya Tanzania, inatambua umuhimu wa kuzingatia masuala ya kijinsia katika sera za fedha, mchakato wa uandaaji wa bajeti, ugawaji wa rasilimali na ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu za Serikali ili kuhakikisha mipango ya kitaifa inachangia katika kujenga uchumi jumuishi na wenye usawa’’ alisema Mhe. Balozi Omar (Mb).

Alisema Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, imezingatia usawa wa jinsia huku Serikali ikiona umuhimu wa kuandaa Taarifa Maalum ya Bajeti inayozingatia Masuala ya Kijinsia (Gender Budget Statement) k**a sehemu ya mfumo rasmi wa usimamizi wa fedha za umma.

Alibainisha kuwa hatua hiyo inaweka msingi wa kuimarisha Mfumo wa Uandaaji wa Bajeti Unaozingatia Masuala ya Kijinsia (GRB), utakaosaidia kuhakikisha masuala ya kijinsia yanaingizwa kikamilifu katika mipango, uandaaji wa bajeti, ugawaji wa rasilimali na ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu za umma.

“Muhimu siyo tu kuangalia kiasi cha fedha kilichotengwa au kutumika, bali pia matokeo yanayopatikana kutokana na rasilimali hizo na kupima matokeo ya matumizi ya fedha za umma’’. Alisema Mhe. Balozi Omar (Mb).

Aliongeza kuwa, katika kuhakikisha rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake zinafuatiliwa kwa ufanisi, mfumo wa Gender Budget Tagging unaopangwa kuanzishwa utakuwa nyenzo muhimu ya kubaini, kufuatilia na kuchambua matumizi ya bajeti yanayolenga masuala hayo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard alisema Wizara ya Fedha ina nafasi muhimu katika kuhakikisha Tanzania inapata na kutoa taarifa zinazohitajika kuhusu Kiashiria cha 5.c.1 cha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 5), kinachopima uwepo wa mifumo ya kufuatilia na kuweka wazi mgao na matumizi ya rasilimali za umma kwa ajili ya kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Alisema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, katika kuimarisha mifumo na uwezo wa kitaasisi unaohitajika ili kuhakikisha masuala ya kijinsia yanaingizwa kikamilifu katika mipango, bajeti na usimamizi wa rasilimali za umma.

Ushirikiano huo unalenga kuimarisha matumizi ya takwimu na taarifa za bajeti katika kufanya maamuzi, kufuatilia rasilimali zinazotengwa kwa masuala ya kijinsia na hatimaye kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaongeza matokeo chanya kwa wananchi, hususan katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi Mbalimbali wa Wizara ya Fedha, akiwemo Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Bw. Melckzedek Mbise, Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Bw. Andambike Mololo pamoja na Wataalamu wengine wa Wizara ya Fedha.

Baraza la Masoko ya Mitaji (Capital Markets Tribunal – CMT) linaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha uendelevu w...
10/08/2026

Baraza la Masoko ya Mitaji (Capital Markets Tribunal – CMT) linaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa upatikanaji wa haki kwa haraka na weledi katika utatuzi wa migogoro inayohusu masoko ya mitaji, dhamana na biashara ya bidhaa nchini.

Likiwa na mamlaka sawa na Mahak**a Kuu katika kushughulikia mashauri ya madai yanayohusu masoko ya mitaji, dhamana na bidhaa; Baraza hilo, ni chombo huru cha kisheria kilichoanzishwa chini ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura ya 79.

Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT) kwenye Manoesho ya Nane Nane 2026, lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Fedha, Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji Tanzania (CMT), Mhe. Dkt. Martin Wilbert Kolikoli, alisema Baraza hilo linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kukuza uchumi wa nchi.

‘’Lengo kuu la kuanzishwa kwa Baraza hii ni kuhakikisha migogoro inayojitokeza katika sekta ya masoko ya fedha inashughulikiwa kwa haraka, kwa haki na kwa kutumia utaalamu maalumu unaozingatia mazingira ya sekta hiyo hivyo tunahakikisha kuwa kwa pamoja tunajenga masoko ya haki, yenye tija katika na kuwa endelevu kuelekea Dira 2050’’ alisema Dkt. Kolikoli.

Alisema uwepo wa Baraza hilo unachangia kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ulinzi wa haki za washiriki wa masoko ya mitaji, huku ukiunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza uchumi kupitia sekta ya fedha na uwekezaji.

‘’Lengo letu ni kuongeza imani na ujasiri katika sekta ya kilimobiashara; kuwawezesha wakulima, vyama vya ushirika na wajasiriamali wa kilimo kutumia kikamilifu na kunufaika na masoko yetu ya bidhaa na hisa, pamoja na mipango ya uwekezaji wa pamoja’’ alisema Dkt. Kolikoli.

Alieleza kuwa CMT inatekeleza jukumu la kusikiliza na kuamua migogoro inayotokana na shughuli za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) pamoja na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (Collective Investment Schemes).

Aliongeza kuwa Baraza hilo lina mamlaka ya kushughulikia mashauri yanayohusu hisa, hati fungani za kampuni, vipande vya uwekezaji (units), mifuko ya uwekezaji inayouzwa sokoni (Exchange-Traded Funds – ETFs), pamoja na biashara ya mazao inayofanyika kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Uuzaji wa TMX.

Alibainisha kuwa Baraza hilo linaongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Jaji wa Mahak**a Kuu ya Tanzania, akisaidiwa na wajumbe wanne wenye utaalamu katika masuala ya sheria na masoko ya mitaji. Shughuli zake za kila siku zinaratibiwa na Sekretarieti inayoongozwa na Msajili.

Moja ya sifa zinazotofautisha Baraza la Masoko ya Mitaji ni kasi ya utoaji wa haki ambapo baada ya usikilizwaji wa shauri kuanza, mchakato mzima wa kulisikiliza na kuliamua hukamilika ndani ya siku 45, hatua inayosaidia kupunguza ucheleweshaji wa mashauri na kuongeza imani ya wawekezaji na wadau wa sekta ya fedha.

Maadhimisho ya Nane Nane 2026 yenye kaulimbiu ‘’Tambua soko ongeza tija kuendeleza Dira 2050, ni Maadhimisho ya 33 ambayo yanalenga kukuza uchumi, kuongeza matumizi ya teknolojia bora na kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa ambayo yanaendelea katika Uwanja wa Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Address

Magufuli City, Treasury Street, Mtumba
Dodoma
40468

Opening Hours

Monday 09:00 - 16:30
Tuesday 09:00 - 16:30
Wednesday 09:00 - 16:30
Thursday 09:00 - 16:30
Friday 09:00 - 16:30

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Wizara ya Fedha posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Organization

Send a message to Wizara ya Fedha:

Shortcuts

Share