15/07/2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa mpira wa miguu Dodoma umefikia asilimia 12, akieleza kuwa eneo la mzunguko la uwanja huo linatarajiwa kufikia asilimia 50 ifikapo Desemba 2026.
Msigwa amesema hayo Julai 15, 2026, alipofanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo unaotarajiwa kubeba mashabiki 32,000 pindi utakapokamilika katika eneo la Nzuguni, jijini Dodoma.
Amesema kuchelewa kwa mradi huo kwa kiasi fulani kumesababishwa na hatua ya Serikali kujiridhisha kuhusu ubora wa kazi inayotekelezwa na mkandarasi pamoja na kuhakikisha miundombinu na vifaa vyote muhimu vinavyohitajika katika uwanja huo vinawekwa kwa viwango vinavyostahili ili kiwango cha fedha zilizotolewa kiendane na ubora wa mradi.
"Ndugu zangu wananchi, pamoja na kwamba tunaye Mkandarasi hatuwezi kutekeleza mradi huu kwa kukurupuka. Lazima tujiridhishe kuhusu ubora wa kazi zinazofanywa na Mkandarasi na kuhakikisha vifaa vyote vinavyotakiwa vimewekwa ili tupate uwanja wa viwango vya kimataifa," amesisitiza Msigwa.
Amesema baada ya majadiliano kati ya Serikali na mkandarasi kukamilika, utekelezaji wa mradi unaendelea kwa kasi na ifikapo Desemba 2026 mradi huo unatarajiwa kufikia asilimia 50, ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa mzunguko wa kwanza wa ujenzi.
"Dodoma ni makao makuu ya nchi, hivyo ni lazima iwe na uwanja unaoakisi hadhi hiyo. Serikali itaendelea kusimamia mradi huu kwa umakini ili kuhakikisha tunapata uwanja wenye ubora tunaoutarajia," amesema Msigwa.
Aidha, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo Desemba 2027 mradi huo unakuwa umekamilika au umefikia hatua za mwisho za ukamilishaji, huku kasi ya ujenzi ikiendelea kuimarika.
Kwa upande wake, Mkandarasi na Mshauri elekezi wa mradi huo, Ashraf Shawky, amesema ifikapo Desemba, 2026 mzunguko wa kwanza wa uwanja wenye uwezo wa kubeba watazamaji 16,000 utakuwa umekamilika, wakati ujenzi wa mzunguko wa pili ukiendelea kwa kasi.
Pia amesema amepokea maelekezo ya Serikali na kuahidi kuhakikisha mradi unakamilika kwa ubora uliokusudiwa na kwa kuzingatia viwango na mahitaji yote muhimu yaliyowekwa.
Mwisho