01/06/2026
🇹🇿
CGP KATUNGU 'ATETA' NA WAJUMBE WA BODI YA TPS SACCOS LTD JIJINI DODOMA
Na SGT. Geofrey Jacka - DODOMA
Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, CGP. Jeremiah Yoram Katungu, amekutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Jeshi la Magereza (TPS SACCOS LTD), katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Magereza, Msalato jijini Dodoma, Juni 01, 2026.
Akizungumza katika kikao hicho, CGP. Katungu, ameipongeza Bodi hiyo na uongozi wa chama kwa usimamizi, uendeshaji na utoaji huduma bora, jambo linalopelekea kutokuwa na malalamiko kutoka kwa wanachama.
Aidha, CGP. Katungu, ameitaka Bodi kuendelea kuwa wabunifu katika utoaji huduma, kutumia vizuri rasilimali za chama, pamoja na kutoa elimu kwa Maafisa na Askari ili waone umuhimu wa kutumia huduma za chama hicho na si vinginevyo.
Kwaupande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPS SACCOS LTD, Kamishna wa Fedha na Mipango, CP. Chacha Bina Jackson, amemshukuru CGP. Katungu kwa malezi mazuri ya Chama hicho, akieleza kuwa ushirikiano anaoutoa kwa Bodi umekuwa chachu ya mafanikio yanayopatikana, ikiwa ni pamoja na ongezeko la akiba za wanachama na mali za chama.
Akisoma Taarifa fupi ya Chama kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Mei 10, 2026, Meneja wa TPS SACCOS LTD, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) John Itambu, amesema kumekuwa na ongezeko la wanachama ambao wamechangia zaidi ya bilioni Mbili, ikiwa ni kiwango cha juu ukilinganisha na bilioni moja zilizopokelewa katika kipindi k**a hicho Mwaka 2025.