Wizara ya Katiba na Sheria

Wizara ya Katiba na Sheria The United Republic of Tanzania
Ministry of Constitutional and Legal Affairs

04/09/2026

SERIKALI YAENDELEA KUPITIA SHERIA KWA AJILI YA DIRA 2050

Serikali imebainisha kuwa inaendelea na zoezi la kupitia sheria mbalimbali nchini ili kuondoa vikwazo dhidi ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050. Hayo yamebainishwa kupitia majibu yaliyotolewa bungeni na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba.

Katika majibu hayo bungeni, Mhe. Katimba ameeleza kuwa timu iliyoundwa na Serikali tayari imeandaa mpango wa kupitia mifumo 28 ya sheria, ambapo kwa sasa inaendelea kupitia mifumo ya sheria za viwanda, biashara, uwekezaji, kodi na nishati.

Ameeleza kuwa vipaumbele vyote saba vya Dira 2050, ikiwemo kilimo na usalama wa chakula, vinazingatiwa katika zoezi hili.

Naibu Waziri Katimba amefafanua kuwa mwaka huu wa fedha, Serikali inatarajia kufanya marekebisho ya mifumo 12 ya sheria za kipaumbele, hatua itakayowezesha sekta binafsi, inayotarajiwa kuchangia asilimia 70 ya uwekezaji katika Dira 2050, kupata mazingira rafiki ya kisheria.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kwenda kwa kasi na vipaumbele ili sheria ziwe tayari na utekelezaji wa Dira 2050 usikwame.

MIFUMO 12 YA SHERIA ZA VIPAUMBELE KUFANYIWA MAREKEBISHO MWAKA 2026/27 KUTEKELEZA DIRA 2050.Serikali imeanza  kufanyia ma...
04/09/2026

MIFUMO 12 YA SHERIA ZA VIPAUMBELE KUFANYIWA MAREKEBISHO MWAKA 2026/27 KUTEKELEZA DIRA 2050.

Serikali imeanza kufanyia marekebisho ya mifumo 12 ya sheria iliyobainika kuwa ya kipaumbele katika mwaka huu wa fedha, ikiwa ni juhudi za kuweka mazingira wezeshi ya kisheria kwa uwekezaji, biashara na maendeleo ya huduma za jamii, kwa mujibu wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Hayo yameelezwa leo Septemba 04, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Mhe. Bahati Kenneth Ndingo, aliyeuliza namna Serikali ilivyojipanga kupitia na kuwasilisha Bungeni mabadiliko ya sheria zinazoweza kuwa kikwazo katika utekelezaji wa Dira hiyo.

Naibu Waziri amesema Serikali inaendelea kupitia sheria mbalimbali nchini kwa lengo la kubaini na kuondoa vifungu au masharti ya kisheria yanayoweza kukwamisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Amesema zoezi hilo linatokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa wakati wa uzinduzi wa Dira 2050, akielekeza Wizara ya Katiba na Sheria, kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania, kufanya tathmini ya sheria na kupendekeza maboresho yanayohitajika.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, Serikali tayari imeandaa mpango wa kupitia mifumo 28 ya sheria, huku zoezi likiendelea katika maeneo ya viwanda, biashara, uwekezaji, kodi na nishati.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Ndingo kuhusu hatima ya sheria zinazohusu kilimo na maendeleo ya jamii, amesema vipaumbele vyote vya Dira 2050 vinazingatiwa katika zoezi hilo, ikiwemo kilimo, usalama wa chakula na rasilimali watu.

Amesema sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya uwekezaji katika utekelezaji wa Dira 2050, hivyo Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa kunakuwa na mfumo wa sheria unaoweka mazingira rafiki kwa sekta hiyo na kuchochea uwekezaji pamoja na shughuli za kiuchumi.

Marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha kuwa sheria zinaendana na mahitaji ya utekelezaji wa Dira 2050, kurahisisha uwekezaji, biashara na uzalishaji, pamoja na kuondoa vikwazo vya kisheria vinavyoweza kuchelewesha maendeleo ya Taifa.

Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kutekeleza zoezi hilo kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa, ili maboresho ya sheria yakamilike kwa wakati na kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zitakazotokana na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

TANZANIA NA RWANDA KUSHIRIKIANA  KATIKA SEKTA YA SHERIATanzania na Rwanda zimekubaliana kushirikiana  katika sekta ya sh...
03/09/2026

TANZANIA NA RWANDA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA SHERIA

Tanzania na Rwanda zimekubaliana kushirikiana katika sekta ya sheria, ikihusisha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, uthibiti wa uhalifu unaovuka mipaka pamoja kuimarisha huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo kati ya Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, na Waziri wa Masuala ya Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Dkt. Emmanuel Ugirashebuja.

Nchi hizo zimekubaliana kubadilishana uzoefu na maarifa katika utatuzi wa migogoro, kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi, hususan wenye uhitaji.

Ushirikiano huu unaonesha dhamira ya Tanzania na Rwanda katika kuimarisha utawala wa sheria, mifumo ya haki na upatikanaji wa haki kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara ya Sheria ya Rwanda jijini Kigali, yakihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe, pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kwa Umma, Ndg. Obadia Kameya.

Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wamepatiwa mafunzo maalumu yenye lengo la kuwajengea uelewa wa kina kuhusu hudum...
03/09/2026

Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wamepatiwa mafunzo maalumu yenye lengo la kuwajengea uelewa wa kina kuhusu huduma, manufaa, na taratibu zinazotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 2 Septemba 2026 jijini Dodoma, yakiongozwa na Maafisa Matekelezo kutoka WCF, Bi. Wende Saga pamoja na Bw. Abdulaziz Mshangani.

DKT. HOMERA ATAKA SHERIA MAHSUSI KULINDA BIASHARA MTANDAOWaziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, ametoa wito ...
02/09/2026

DKT. HOMERA ATAKA SHERIA MAHSUSI KULINDA BIASHARA MTANDAO

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, ametoa wito kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kufanya utafiti kuhusu uanzishwaji wa Sheria mahsusi ya Biashara Mtandao (E-Commerce Law) kwa lengo la kuweka mazingira ya kisheria yaliyo salama, rafiki na yenye uhakika kwa biashara na uwekezaji wa kidijitali, kukuza ubunifu na ushindani, kulinda wafanyabiashara pamoja na kuiwezesha nchi kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Dkt. Homera ametoa wito huo 2 Septemba, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha kujadili hatua zilizofikiwa katika maboresho ya sheria kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kilichowakutanisha Waziri wa Katiba na Sheria na Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bw. George Nathaniel Mandepo.

“Kutokana na mabadiliko ya teknolojia, kukua kwa Uchumi wa kidijitali pamoja na kuongezeka kwa biashara mtandao kuna umuhimu sasa wa kuwa na mfumo wa kisheria unaoendana na mazingira ya sasa na yanayotarajiwa ya uchumi wa kidijitali’’ alisema Dkt. Homera.

“Sambamba na hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha uchumi wa kidijitali, mnapaswa kuanza kufanya utafiti na kuwasilisha mapendekezo yatakayoiwezesha Serikali kufanya uamuzi wa kisera na kisheria kuhusu haja ya kutungwa kwa Sheria mahsusi ya Biashara Mtandao au kufanya maboresho stahiki katika sheria zilizopo’’ aliongeza Dkt. Homera.

Dkt. Homera alisema utafiti huu unatarajiwa kuchambua sheria zilizopo, kubaini changamoto za kisheria, pamoja na kufanya ulinganisho na mifumo ya sheria na uzoefu wa nchi nyingine katika kusimamia biashara mtandao.
Hatua hiyo

Aidha, Dkt. Homera amebainisha kuwa hatua hii ya utafiti ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuimarisha mfumo wa kisheria unaoendana na mabadiliko ya teknolojia, pamoja na kuweka mazingira bora kwa ukuaji wa biashara na uchumi wa kidijitali katika sekta zote ikiwemo sekta ya biashara yam azo ya kilimo nchini.

Maeneo yanayotarajiwa kupewa kipaumbele katika utafiti huo ni pamoja na mikataba ya kielektroniki, ulinzi wa watumiaji, usimamizi wa majukwaa ya kidijitali, malipo ya kielektroniki, ulinzi wa taarifa binafsi, usalama wa miamala, haki miliki, masuala ya kodi, ushindani pamoja na utatuzi wa migogoro ya biashara mtandao.

02/09/2026

MABADILIKO YA SHERIA KUFUNGUA FURSA MPYA ZA MIKOPO KWA VIJANA

Serikali imesema mabadiliko ya sheria yamefungua fursa mpya kwa vijana kupata mikopo kwa kutumia mali zinazohamishika na zisizohamishika k**a dhamana.

Akijibu swali la Mheshimiwa Timida Mpoki Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum (Vijana), kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya vijana Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba,alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuwawezesha vijana kupata mitaji na ujuzi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia.

Alisema fursa hiyo imepatikana baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika ya mwaka 2026, inayoruhusu mali zinazoshikika na zisizoshikika kutumika k**a dhamana ya mikopo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mhe. Katimba Kifungu cha Nane cha sheria hiyo kimeainisha aina za mali zinazoweza kuwekwa dhamana, hatua inayolenga kuondoa changamoto ya vijana kutakiwa kuwa na mali zisizohamishika pekee ili kupata mikopo katika taasisi rasmi za kifedha.

Alisema utekelezaji wa sheria hiyo unatarajiwa kuwawezesha vijana kupata mitaji ya kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Aidha, Naibu Waziri Katimba alisema Serikali imeendelea kurahisisha masharti ya mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (Youth Development Fund), pamoja na mikopo inayotolewa kupitia ahadi ya Shilingi bilioni 200. Katika mpango huo, vifaa vinavyotolewa kwa vijana vinaweza kutumika k**a dhamana ya mikopo.

Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kupunguza masharti ya dhamana katika mikopo inayotolewa na Halmashauri kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani.

Hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, toleo la 2024, pamoja na Mkakati wake wa Utekelezaji wa mwaka 2024–2034, unaolenga kukuza ajira, ujasiriamali na uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana.

Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupata mitaji, ujuzi na fursa za kiuchumi, pamoja na kuhakikisha wanapata ujuzi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia ili waweze kujiajiri, kuajiri wengine na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

02/09/2026

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amewataka makamishna wapya wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakikisha sheria za nchi zinaendana na mahitaji na mazingira ya Watanzania.

Dkt. Homera ameyasema hayo Septemba 1, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo elekezi kwa makamishna hao, huku akiwasitiza kuwa hakuna taifa imara bila kuwa na sheria imara zinazolinda haki, kuchochea maendeleo na kuwezesha mazingira bora ya uwekezaji nchini.

Aidha Dkt. Homera amewashukuru makamishna wanaomaliza muda wao kwa mchango walioutoa, akiwataka kuwa tayari kutoa ushauri na kushirikiana na Tume mpya pale watakapohitajika.

HOMERA: HAKUNA TAIFA IMARA BILA SHERIA IMARAMakamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, wametakiwa kutumia uzoefu...
01/09/2026

HOMERA: HAKUNA TAIFA IMARA BILA SHERIA IMARA

Makamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, wametakiwa kutumia uzoefu na maarifa waliyonayo kuhakikisha Taifa linakuwa na sheria bora zitakazosaidia katika kutekeleza Dira 2050.

Hayo yamewekwa bayana na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera wakati akifungua mafunzo elekezi kwa Makamishna wapya wa ofisi ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania yaliyofanyika leo 01 Septemba, 2026, jijini Dodoma

Dkt. Homera amesema serikali imekua ikikutana na changamoto ya utekelezaji wa sheria ambazo hazijafanyiwa utafiti, jambo linalopelekea kuwa na sheria zilizopitwa na wakati na kuzitaka wizara na taasisi kabla ya kutunga au kubadili sheria kushirikiana na Tume kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Waziri Homera amesema hakuna Taifa imara bila kuwa na sheria imara na zenye tija kwa Taifa, na amewapongeza Makamishna waliomaliza muda wao na kuwataka Makamishna wapya kumsaidia Mhe. Rais katika kuhakikisha Sheria za Nchi zinaendana na wakati hasa katika kutekeleza Dira 2050.

"Hakuna Taifa imara bila kuwa na sheria imara zenye tija kwa Taifa letu na watanzania kwa ujumla ".Alisema Dkt. Homera.

Awali, akimkaribisha Mhe. Waziri, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Jaji Winfrida Korosso, amesema Tume imejipanga vyema kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuishukuru Wizara kwa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya Tume, hatua iliyowezesha ufanisi wake.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeundwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania sura 171 na majukumu yake yameainishwa katika kifungu cha 4 cha sheria hiyo ikiwa na lengo la kuhakikisha nchi inakuwa na sheria himilivu na zinazoakisi mazingira ya Tanzania.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, leo Septemba 1, 2026, amekutana na viongozi wa Taasisi ya Cult...
01/09/2026

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, leo Septemba 1, 2026, amekutana na viongozi wa Taasisi ya Culture and Development East Africa, Bi. Ayeta Wangusa na Ndugu Madaraka Nyerere, katika Ofisi ya Waziri iliyopo katika jengo la Tume ya Utumishi wa Mahak**a zilizopo katika Tambukareli, jijini Dodoma.

Katika kikao hicho viongozi hao wamejadiliana fursa na njia za kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi hiyo, hususan katika maendeleo ya sekta ya filamu na maudhui ya sauti na picha (audiovisual content), ambayo ni sehemu muhimu ya kukuza uchumi wa ubunifu.

Katika hatua nyingine pande zote mbili zimeonesha nia ya kuendeleza mazungumzo na ushirikiano kwa lengo la kuimarisha tasnia ya filamu na maudhui ya sauti na picha nchini na kukuza ushirikiano wa kikanda katika sekta ya ubunifu Afrika Mashariki.

TAARIFA KWA UMMA
01/09/2026

TAARIFA KWA UMMA

Address

Government City, Mtumba
Dodoma
41207

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Wizara ya Katiba na Sheria posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Shortcuts

Share