02/07/2026
WATERAID YAKABIDHI MRADI WA MAJI WA SH. MILIONI 465 HANDENI MJI
Na Job Karongo - Handeni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, leo Julai 2, 2026, amepokea rasmi Mradi wa Usambazaji wa Huduma ya Maji ya Mtandao wa Bomba wa Kwamaizi uliotekelezwa katika Kata ya Kideleko, Halmashauri ya Mji Handeni, Mkoa wa Tanga.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mhandisi Waziri amesema Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi ili kuboresha afya na ustawi wa wananchi.
Mradi huo uliotekelezwa na WaterAid Tanzania kwa ufadhili wa OKF, kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, RUWASA, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni (HTM) pamoja na Halmashauri ya Mji Handeni, umetumia Shilingi Milioni 465,182,915.20 TZS na unatarajiwa kunufaisha wananchi 6,037 wa maeneo ya Kideleko, Kampene, Muungano, Ndekai na Bangu.
Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chujio la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000, tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 100,000, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji lenye urefu wa mita 1,485, uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa mita 2,358, pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji vyenye mfumo wa malipo ya kabla.
Mhandisi Waziri amesisitiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni (HTM), RUWASA, viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi kuendelea kulinda, kutunza na kusimamia miundombinu hiyo ili huduma ya maji iendelee kuwa endelevu na kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Bi. Anna Mzinga, ameitaka RUWASA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni (HTM) pamoja na Halmashauri ya Mji Handeni kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza na kupanua huduma za mradi huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mkurgugenzi huyo amebainisha kuwa usimamizi bora wa miundombinu wa mradi huo utahakikisha uwekezaji uliofanywa unaendelea kuleta matokeo chanya kwa muda mrefu.