04/07/2023
WAZIRI WA MADINI MHE. DKT DOTTO MASHAKA BITEKO AFUNGUA ZAHANATI YA KIJIJI NYAMISHIGA
Julai 3, 2023
Waziri wa Madini nchini Mheshimiwa Dkt Dotto Mashaka Biteko jana amefungua zahanati na kukabidhi gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) katika Kijiji cha Nyamishiga, Kata ya Lunguya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Akizungumza katika ufunguzi wa zahanati hiyo Mhe Dkt Biteko amewapongeza Kikundi cha Wanawake wachimbaji wadogowadogo (TAWOMA-MSHIK**ANO) ambacho kilijitolea kutekeleza ujenzi wa Zahanati hiyo pamoja na kununua gari vyote vikiwa na thamani ya Tsh Milioni 289.
Mbali na kukishukuru kikundi hicho Dkt Biteko pia amewapongeza Viongozi mkoani Shinyanga kwa namna wanavyotetea na kusimamia maslahi ya wachimbaji wadogowadogo. "Kwa Shinyanga hakika mna viongozi makini sana, mnaye Mama Mndeme mkuu wa Mkoa huu anapambana sana kuwatetea wachimbaji, kwahilo nampongeza sana lakini pia mnaye Mkuu wenu wa Wilaya Mhe Mboni anachapa kazi haswa, watu hawa hawalali kwa ajili ya kuwatetea ninyi." Amesema Dkt Biteko.
"Kipekee kabisa nimpongeze na nimshukuru sana Mbunge wa Jimbo hili Mhe Iddi Kassim Iddi anahangaika mno kuwapigania wachimbaji hawa, amekuwa akinifuata kila mara kunieleza changamoto mnazokutana nazo nami nashirikiana naye katika kutatua changamoto hizo na kiukweli Mbunge wenu anastahili pongezi nyingi sana kwenye hili" Aliongeza Dkt Biteko.
Aidha, Dkt Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha sekta ya Madini nchini hususani kundi la wachimbaji wadogowadogo ambao hapo awali walionekana hawawezi kuendesha shughuli za uchimbaji lakini chini ya utawala wake ametoa kipaumbele kwa kundi hilo na mafanikio yanaonekana.
Awali akimkaribisha Mhe.Dkt Biteko Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Christina Mndeme amemshukuru Waziri huyo kwa kutenga muda kuja Shinyanga na kuwaunga mkono katika shughuli hiyo ambapo pia alimuomba afikishe shukrani za Mkoa huu kwa Rais Dkt Samia kutokana na fedha nyingi za maendeleo alizozileta katika mkoa huu.