18/06/2026
Diwani wa Kata ya Usinge, Mhe. Kulwa M. Kajoro, amehitimisha rasmi ziara yake ya siku saba ndani ya Kata ya Usinge kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara katika eneo la Usinge Kati. Katika ziara hiyo, aliambatana na viongozi mbalimbali pamoja na maafisa wa kata kwa lengo la kusikiliza, kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Ziara hiyo imekuwa jukwaa muhimu lililowapa wananchi nafasi ya kueleza kero zao moja kwa moja kwa viongozi, jambo ambalo limeongeza matumaini na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na uongozi wa kata.
Miongoni mwa masuala yaliyopatiwa ufafanuzi na hatua za utatuzi ni pamoja na huduma za afya, elimu, usalama barabarani, migogoro ya uharibifu wa mazao unaosababishwa na mifugo, ujenzi wa machinjio ya kisasa, eneo la muda la maegesho ya mabasi, uchongaji wa barabara za mitaa, matumizi sahihi ya vyoo vya soko, upanuzi wa huduma za umeme katika vitongoji na mitaa pamoja na huduma ya ukusanyaji wa taka katika soko la Usinge.
Wananchi wengi wameeleza kuridhishwa na ziara hiyo, wakisema imewapa fursa ya kuwasilisha changamoto zao kwa uwazi na kupata majibu ya moja kwa moja kutoka kwa viongozi. Baadhi ya vijana wa Usinge walimpongeza Mhe. Kajoro kwa kuanzisha utaratibu huo na kumuomba aendelee kuitisha mikutano ya hadhara mara kwa mara ili kuimarisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi.
Akizungumza katika mkutano wa kuhitimisha ziara hiyo, Mhe. Kajoro aliwashukuru wananchi wote kwa kujitokeza kwa wingi na kwa kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni, kero na mapendekezo yao. Aliwahimiza kuendelea kushirikiana na viongozi wa kata na kujitokeza kwa wingi zaidi katika mikutano ijayo ili kwa pamoja wajenge maendeleo endelevu ya Kata ya Usinge.
Ziara hiyo ya siku saba imeweka historia ya kuwa ziara ya kwanza kwa Diwani wa Kata ya Usinge kuzunguka vijiji na vitongoji vyote vya kata hiyo akiwa pamoja na viongozi na maafisa wa kata, kwa lengo la kusikiliza wananchi, kutatua changamoto zao na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
"Maendeleo ya Usinge yatachangiwa na ushiriki wa wananchi wenyewe. Tukisikilizana, tukishirikiana na kutatua changamoto kwa pamoja, tutafikia maendeleo tunayoyataka." – Mhe. Kulwa M. Kajoro.
Imetolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano
Ofisi ya Diwani Kata ya Usinge