29/05/2026
Watumishi wa Makao Makuu ya Halmashauri jana Mei 28, 2026, wamepatiwa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili pamoja na maambukizi ya VVU katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya za watumishi ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Elimu hiyo iliyotolewa na wataalamu wa afya ilijikita katika uelewa wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu (presha), kisukari, magonjwa ya kifua, selimundu, saratani na changamoto za afya ya akili.
Wataalamu hao wamesisitiza umuhimu wa kuboresha mitindo ya maisha kwa kufanya mazoezi mara kwa mara, kula lishe bora, kupunguza matumizi ya pombe na tumbaku pamoja na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kutambua hali zao mapema.
Aidha, washiriki wameelimishwa kuhusu visababishi vya maambukizi ya VVU, njia za kujikinga pamoja na umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara.
Pia, wajumbe wamepata mafunzo ya namna ya kutumia vifaa vya kujipima VVU wenyewe majumbani (self-test), huku vipimo hivyo vikigawiwa kwa watumishi walioonyesha uhitaji.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Ezekiel Ntiriyo amewataka watumishi kuweka kipaumbele katika kulinda afya zao, akieleza kuwa mtumishi mwenye afya njema ana uwezo mkubwa wa kutoa huduma bora, kwa wakati na kwa ufanisi kwa wananchi.
“Afya ya mtumishi ni msingi wa utendaji kazi wenye tija. Ni muhimu kila mmoja kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa ili kuendelea kulitumikia taifa kwa ufanisi,” amesisitiza.