17/07/2026
KAMATI ZA SHULE, WAZAZI NA VIONGOZI WA DINI BUSOKELO WAPOKEA MRADI WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI.
Kamati za Shule, wawakilishi wa Wazazi pamoja na wawakilishi wa Viongozi wa Dini kutoka Shule ya Msingi Mbambo iliyopo Kata ya Kambasegela na Shule ya Msingi Itete iliyopo Kata ya Itete, Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo, wamepokea kutambulishwa kwa Mradi wa Unywaji Maziwa Shuleni unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Oktoba 2026.
Zoezi la utambulishaji wa mradi huo limefanyika leo 17/07/2026 na kuongozwa na Dkt. Mackrina Nombo, Mtaalamu wa Lishe kutoka Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi, ambao unatekelezwa chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ufadhili wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
Akizungumza wakati wa utambulishaji huo, Dkt. Nombo amesema lengo kuu la mradi ni kuboresha kipato cha wafugaji na wananchi, kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuboresha lishe, hususan kwa watoto wa shule za msingi kupitia programu ya unywaji maziwa shuleni.
Programu hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha afya na maendeleo ya wanafunzi kwa kuhakikisha wanapata lishe bora, kupunguza utapiamlo na udumavu, kuongeza umakini darasani na hatimaye kuchangia kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi.
Katika kikao hicho, Kamati za Shule, Wawakilishi wa Wazazi na Viongozi wa Dini walipatiwa elimu kuhusu utekelezaji wa mradi na wajibu wa kila mdau katika kuhakikisha unafanikiwa. Viongozi wa Dini walisisitiza umuhimu wa kuwaelimisha wanafunzi kuhusu faida za unywaji wa maziwa, huku wakihimiza wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono utekelezaji wa mradi huo.
Aidha, washiriki walielezwa kuwa mradi huo utasaidia kukuza uzalishaji wa maziwa, kuongeza soko la maziwa kwa wafugaji, kuhamasisha utamaduni wa unywaji maziwa shuleni na kuboresha hali ya lishe kwa watoto, hatua itakayochochea maendeleo ya sekta ya mifugo na kuinua ustawi wa jamii kwa ujumla.
Mradi wa Unywaji Maziwa Shuleni unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Oktoba 2026, ukiwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha lishe kwa wanafunzi na kukuza uchumi wa wafugaji kupitia sekta ya maziwa.