24/04/2023
Uongozi wa Bodi ya kahawa - TCB, umeahidi neema nyingine kwa wakulima na wadau wa KAHAWA nchini, muda si mrefu itaendelea na zoezi la ugawaji wa miche bora ya kahawa.
Hayo yamesemwa na Bw.Shamba mkuu wa Bodi hiyo, Ndg Kajiru, wakati akitolea ufafanuzi wa moja ya hoja na maswali kutoka kwa wadau wa mkutano huo kuhusu miche bora.
Aidha Bw.Kajiru aliyemuwakilisha mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Ndugu Primus Kimaryo, amesema kuwa bosi tayari imeshafanyia kazi changamoto hiyo na tayari imeshaanza utekelezaji wake na inatarajia hivi karibuni kuendelea na zoezi hilo la ugawaji wa miche bora na ya kisasa, kwa wakulima kupitia vyama vyao vya msingi-Amcos, hivyo ni suala la muda tu ila watagawa kulinagana na mahitaji ya mwanzo wa msimu.
Ameongeza kuwa Bodi ya Kahawa, imeendelea na zoezi la ugawaji miche bure kwa wakulima wa kahawa nchini ikiwa ni moja ya jitihada za kuongeza uzalishaji kufikia tani 300,000 mwaka 2025.
Hatua hii inalenga kufikia lengo la uzalishaji na ugawaji miche milioni 20 kila mwaka, ambapo hadi kufikia Aprili 2023 jumla ya miche zaidi ya 8,784,146, imegawiwa katika msimu wa 2022/2023.
Mwisho ametoa wito kwa wakulima wa Kahawa kote nchini, kufuata kanuni na misingi ya Wizara ya Kilimo, ambapo amewashauri kupeleka mazao yao kwenye AMCOS, ili kupata bei nzuri na elekezi.
Amewaahidi kuwa Bodi itazidi kuboresha mfumo na mazingira wezeshi kwa wakulima na wadau nchini, ikiwemo kutangaza bei za kahawa za kidunia kila siku kupitia vyombo mbalimbali vya habari hasa kupitia mitandao yake ya kijamii.