10/06/2025
MKUTANO MKUU WA KIJIJI CHA TUKAMISASA WAAZIMIA MWENYEKITI KUPISHA UCHUNGUZI
Na John Mlyambate
Kijiji cha Tukamisasa, wilayani Bagamoyo, kimetawaliwa na mvutano mkubwa baada ya Mkutano Mkuu wa Kijiji hicho, uliofanyika hivi karibuni, kuazimia Mwenyekiti wa Kijiji, Bwana Ramadhani Zahaki, asimame kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili.
Mkutano huo uliitishwa na Mwenyekiti Zahaki mwenyewe kwa lengo la kujadili na kupokea kero mbalimbali za wananchi, na kufanyika katika ofisi ya kijiji hicho mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mheshimiwa Shaibu Ndemanga.
Katika kikao hicho, wananchi walipata nafasi ya kueleza matatizo yao hadharani, ambapo Bwana Malaki Mamungiti, ambaye ni Mwenyekiti wa wafugaji wa kijiji hicho, aliibuka na tuhuma nzito dhidi ya Mwenyekiti Zahaki, akidai amekuwa akijimilikisha ardhi ya kijiji kinyume cha sheria.
Malaki alidai kuwa Mwenyekiti huyo anamiliki zaidi ya ekari 500 ambazo anazidai kuwa ni za familia yake, akitumia nafasi yake vibaya kwa maslahi binafsi, jambo linalokiuka taratibu za kisheria na kiutawala.
Mbali na suala la ardhi, Malaki alieleza kuwa Mwenyekiti huyo amekuwa akiwaingiza wawekezaji kwenye vitega uchumi vya kijiji bila idhini ya vikao halali, huku akijipatia mapato yasiyo halali bila uwazi au ufuatiliaji wa fedha hizo.
Wananchi wengine pia walitoa tuhuma mbalimbali, akiwemo Mzee Mathias Mkundi, ambaye alisema kuwa Mwenyekiti Zahaki hana ushirikiano na Mtendaji wa Kijiji pamoja na Halmashauri ya Kijiji, hali inayozorotesha utendaji wa serikali ya kijiji.
Mzee Mkundi alieleza kuwa hakujawahi kufanyika kikao chochote cha kisheria tangu Mwenyekiti huyo aingie madarakani, hali inayomnyima mamlaka na sauti ya wananchi katika maamuzi ya kijiji.
Kwa upande wake, Mzee Ismail Lugoma, alieleza kuwa Mwenyekiti hajawahi kusoma mapato na matumizi ya kijiji hadharani, licha ya kijiji hicho kuwa na vyanzo vingi vya mapato vinavyoendelea kukusanya fedha.
Mzee Lugoma alipendekeza kuwa ni busara kwa Mwenyekiti Zahaki kupisha uchunguzi ili ukweli ubainike na hatua stahiki zichukuliwe, kwa kuwa hali ya sasa inarudisha nyuma maendeleo ya kijiji hicho.
Wananchi waliunga mkono hoja hiyo kwa kauli moja, wakimtaka Mkuu wa Wilaya kuingilia kati na kuhakikisha tume huru inaundwa kuchunguza tuhuma hizo, kwa lengo la kulinda maslahi ya umma na kurejesha imani ya wananchi kwa uongozi.
Kutokana na hali hiyo, Mkutano Mkuu wa Kijiji cha Tukamisasa uliamua rasmi kwamba Mwenyekiti Zahaki asimame kazi kwa muda, hadi uchunguzi kamili ufanyike, na walimkabidhi rasmi ombi hilo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo.
Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Shaibu Ndemanga, alikubaliana na ombi hilo na kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, ambaye aliiwakilishwa katika kikao hicho na Afisa Utumishi, kuunda tume ya uchunguzi mara moja.
Tume hiyo itapitia na kuchunguza tuhuma zote zilizotolewa na wananchi, zikiwemo za matumizi mabaya ya madaraka, ubaguzi, ukabila, ubadhirifu wa mali ya kijiji na uvunjaji wa taratibu za kiutawala.
Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwa tume hiyo itafanya kazi kwa weledi na itatoa ripoti ya uchunguzi mbele ya Mkutano Mkuu wa Kijiji cha Tukamisasa kwa ajili ya hatua zaidi, kuhakikisha haki na uwajibikaji vinazingatiwa.
Wananchi wa Tukamisasa walionyesha matumaini kuwa hatua hiyo ya kusimamishwa kwa Mwenyekiti Zahaki itasaidia kurejesha utawala bora na uwazi katika uongozi wa kijiji chao.