02/07/2026
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ya Maandalizi ya AFCON 2027, Dkt. Jim Yonazi, ameowangoza Makatibu Wakuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ziara ya ukaguzi wa maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 hiyo Zanzibar.
Kamati ilitembelea Uwanja wa New Amaan Complex na uwanja mpya unaojengwa Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo Dkt. Yonazi amesema maendeleo ya ujenzi na ukarabati yanaendelea vizuri ili kuhakikisha viwanja hivyo vinakidhi viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti inayohusisha ujenzi na ukarabati wa viwanja, uboreshaji wa miundombinu ya barabara, usalama na utangazaji wa vivutio vya utalii, kwa lengo la kuongeza uwekezaji, ajira na kuimarisha uchumi kupitia AFCON 2027.
"AFCON 2027 si mashindano ya soka pekee, bali ni fursa ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi," amesema Dkt. Yonazi.
Aidha, ametoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa zitakazotokana na mashindano hayo, hususan katika sekta za utalii, hoteli na huduma nyingine.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Bw. Salhina Mwita, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na ukarabati wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumiwa na timu shiriki na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Muungano ili kuhakikisha maandalizi ya AFCON 2027 yanafanikiwa kwa viwango vinavyohitajika.