28/02/2020
Imewekwa: February 27th, 2020
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Ndg.Richard Kwitega amewataka Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Wilayani Arumeru, mkoani humo kutekeleza wajibu wao kuendana na kasi ya awamu ya tano iliyojikita kwenye utawala bora na kuwaletea wananchi maendeleo .
Kwitega amesema hayo Wakati wa Ziara yake katika Halmashauri hiyo inayolenga kukumbusha wajibu na utendaji ,kuona changamoto zinazowakabili Watumishi na namna ya kuzitatua, ambapo amesema watumishi hao hawana budi kutimiza majukumu yao kwa weledi na ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora ili kuwaletea maendeleo wananchi "kila Mtumishi wa umma ana umuhimu kwa nafasi aliyonayo katika swala la maendeleo " amesema Kwitega
Kwitega ametoa wito kwa Watumishi hao kuwa na maadili ndani na nje ya vituo vyao vya kazi ikiwa ni kuepuka rushwa ,ulevi wa kupindukia pia amekemea kitendo cha baadhi ya watumishi kukopa mitaani kwa dhamana ya kadi zao za benki badala yake wakope kwenye taasisi za fedha kwa utaratibu wa kukopesha Watumishi wa Umma uliowekwa na Serikali "kopeni kwa utaratibu kuepuka kudhalilisha Utumishi wa Umma" amesisitiza Kwitega
Aidha Ndg.Kwitega amewapongeza Watumishi wa Wilaya ya Arumeru kwa utendaji wao unatia fora na kuwezesha Wilaya hiyo kufanya vizuri kwenye Sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Elimu ambapo katika matokeo kidato cha sita mwaka 2019 Shule zake mbili zilifanya vizuri ambapo Shule ya Sekondari Kisimiri ilishika nafasi ya kwanza kitaifa na Shule ya Sekondari Mwandeti ilishika nafasi ya Nne..
Akihitimisha Kwitega amewataka watumishi hao kujitathimini kwa nafasi walizo nazo ni kwa namna gani wametekeleza wajibu wao ili kuwaletea maendeleo
Awali Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimaliwatu. Ndg. David Lyamongi amesema Utumishi wa Umma unaongozwa kwa Sheria na Taratibu ambapo aliweka bayana utaratibu wa stahiki za watumishi wa Umma ikiwa ni upandaji wa madaraja na ubadilishaji vyeo, uhamisho, posho mbalimbali katika utumishi wa Umma , utaratibu wa likizo na ushughulikiaji na ulipaji wa madeni ya watumishi.Ambapo ametoa wito kwa Viongozi na Watumishi kuzingatia Sheria na Taratibu hizo.
Naye katibu tawala wa Wilaya ya Arumeru Mwl. James Nchembe amemshukuru Katibu Tawala Mkoa wa Arusha kwa kupongeza utendaji wa Wilaya hiyo yenye watu zaidi ya laki saba na kuahidi kuendelea kufanya kazi kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.
ziara ya Katibu tawala Mkoa wa Arusha katika Wilaya ya Arumeru imekamilika katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru ambapo Katibu Tawala amezungumza na watumishi wa tarafa za Poli, Mbuguni na King’ori na itaendeleo siku ya Pili katika Halmashauri ya Arusha.
Baadhi ya watumishi waliopata fursa ya kutoa maoni wamepongeza kitendo cha Katibu Tawala Mkoa wa Arusha kufanya ziara hiyo ya kuwakumbusha wajibu wao sambamba na kupokea changamoto walizonazo na kuzitatua na kuomba vikao k**a hivyo kuwa endelevu kuanzia ngazi ya Halmashauri "tunaomba vikao vya namna hii kuendelea kuwepo kwa ngazi mbalimbali kwani vitaleta tija kwenye utendaji wetu " alisihi Ndg. Erick Kulindwa ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Kingori .
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Ndg.Richard Kwitaga akizungumza na Watumishi wa Tarafa ya Poli na Mbuguni katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru .