04/09/2026
MADIWANI JIJI LA DAR WAPITISHA MPANGO MKAKATI WA UBIA (PPP) KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS.
Na:Shalua Mpanda
Baraza la Madiwani la Halmashuri ya Jiji la Dar es salaam kwa kauli moja wamepitisha azimio la kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha Jiji hilo linakuwa safi kwa kushirkisha sekta binafsi katika zoezi la usafishaji wa Mazingira na uzoaji wa taka katika Halmashuri hiyo.
Akizungumza katika Baraza hilo maalum Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ndugu Elihuruma Mabelya amesema kutokana na ongezeko kubwa la watu katika Jiji la Dar es salaam, uzalishaji wa taka umeongezeka hali inayofanya maeneo mengi kuwa na mrudikano wa taka.
Mkurugenzi Mabelya aliomba Baraza hilo kuridhia mchakato wa kuingia ubia kati ya Halmashauri na sekta binafi ili kuweza kumpata mkandarasi atakayekuwa na uwezo wa kufanya kazi ya kukusanya na kuhudumia dampo la Pugu.
"Ni ukweli usiopingika kuwa uondoshaji wa taka katika Halmashuri ya Jiji letu hauendani na kasi ya uzalishaji wa taka hizo, hivyo mpango huu wa PPP (Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi) hatuwezi kuuepuka, hivyo naomba mridhie mpango huu". Alisisitiza Mkurugenzi Mabelya
Diwani wa kata ya Ukonga Mhe. Ramadhan Bendera ameusifu mpango huo huku akitolea mfano wa hali halisi ya dampo la Pugu kuzidiwa kwa kukosa wakandarasi wenye uwezo ambao wanaweza kuhudumia dampo hilo.
Baada ya Mkurugenzi huyo wa Jiji kuomba Baraza hilo kupitisha ajenda hiyo, Madiwani wote waliafiki pendekezo hilo na kuruhusu timu ya menejimenti ya Halmashauri kuendelea na mchakato huo.
Ikumbukwe hivi karibuni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kuapisha baadhi ya viongozi aliowateua, pamoja na mambo mengine alionesha kuchukizwa na hali ya uchafu katika maeneo mengi ndani ya mkoa wa Dar es salaam na kuagiza viongozi kusimamia suala la usafi kwenye maeneo yao.