01/08/2026
Maafisa 21 wa TFS wahitimu mafunzo ya kijeshi, watakiwa kuimarisha uzalendo na nidhamu
Katavi. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umewataka maafisa wake waliokamilisha mafunzo ya mfumo wa kijeshi (Paramilitary Transformation Course) kuyatumia maarifa, uzalendo, nidhamu na uadilifu walioupata katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Wito huo umetolewa jana Julai 31, 2026 na Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Huduma Saidizi, DCC Emmanuel Wilfred Kiboko, wakati akifunga rasmi mafunzo ya Paramilitary Transformation Course Awamu ya 12 yaliyofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Jeshi la Uhifadhi Mlele, mkoani Katavi, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo.
DCC Kiboko aliwapongeza washiriki kwa kuonesha nidhamu na kujituma katika kipindi chote cha mafunzo huku akiwataka kuendeleza misingi hiyo wanaporejea katika vituo vyao vya kazi.
"Mafunzo haya yatawajengea uwezo, yatawajengea uzalendo na yatawajengea uadilifu mtakapokwenda kutekeleza majukumu yenu katika maeneo yenu ya kazi," alisema Kiboko kabla ya kutangaza rasmi kufungwa kwa mafunzo hayo.
Awali, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Mhasibu Mkuu wa TFS, Peter Mwakosya, aliwapongeza wakufunzi wakiongozwa na Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi Mlele, SCO Samuel Msuva, kwa ubunifu na kiwango cha juu cha mafunzo waliokitoa, akisema yameendelea kuboreshwa kila mwaka.
Aliwataka wahitimu kuendeleza nidhamu waliyoijenga kambini akisisitiza kuwa msingi mkuu wa mfumo wa kijeshi ni utii na kwamba mafunzo hayo yataisaidia TFS kujenga taasisi yenye viongozi wenye uwezo mkubwa wa kusimamia rasilimali za taifa.
"Msingi mkuu wa mfumo wa kijeshi ni utii. Tunaamini utii huu pamoja na ukak**avu mliojengewa hapa mtauendeleza mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi ili kuendelea kuijenga TFS imara," alisema Mwakosya.
Akitoa taarifa ya mafunzo, Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi Mlele, Mhifadhi Mwandamizi Samuel Msuva, alisema jumla ya maafisa 21 walihitimu mafunzo hayo, wakiwemo makamishna wanne na maafisa 17, ambapo wanawake walikuwa 12 na wanaume tisa.
Alisema washiriki walipatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo yaliyohusisha uongozi, parade, mazoezi ya viungo, afya, matumizi ya silaha ndogo, mafunzo ya kurusha risasi pamoja na sheria na nyaraka zinazoongoza utendaji wa Jeshi la Uhifadhi.
Kwa mujibu wa Msuva, lengo la mafunzo hayo lilikuwa kuwaandaa viongozi wenye uwezo wa kusimamia askari na watumishi chini yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za mfumo wa kijeshi unaotekelezwa katika taasisi za Jeshi la Uhifadhi.
Aliwataka wahitimu kuwa viongozi wa mfano kwa kuonesha nidhamu, uaminifu, kulinda siri za taasisi na kujenga mshik**ano kazini.
"Panapokuwa na upendo kuna umoja, panapokuwa na umoja kuna nguvu, na penye nguvu hakuna changamoto isiyoweza kushindwa," alisema.
Kwa niaba ya wahitimu, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Meneja Uhusiano wa TFS, Johari Kachambwa, alisema mafunzo hayo yamewaongezea maarifa, stadi na maadili ya kijeshi yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Alisema washiriki wamejengewa uwezo katika nidhamu, itifaki za kijeshi, matumizi salama ya silaha, usimamizi wa watumishi pamoja na utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi kwa kuzingatia sheria na amri za jumla za Jeshi la Uhifadhi.
Kachambwa aliwashukuru viongozi wa TFS kwa kuwezesha watumishi walioajiriwa kabla ya mabadiliko ya mfumo wa taasisi pamoja na wale waliohamia kutoka taasisi zisizo za kijeshi kupata mafunzo hayo maalumu ili kuendana na mfumo wa sasa wa utendaji.
"Tunawaahidi viongozi wetu kuwa tutatumia maarifa, ujuzi na maadili tuliyojifunza kutekeleza majukumu yetu kwa uadilifu, nidhamu, weledi na kujituma kwa maslahi ya taasisi na taifa," alisema.
Picha zaidi link: https://drive.google.com/drive/folders/1XL1hf1eHYmd46vjo-nAVSq9t13NAlTqX?usp=sharing