08/06/2026
KINONDONI YAIDHINISHA MPANGO MKAKATI WA KUPUNGUZA TAKA ZA PLASTIKI
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeidhinisha Mpango Mkakati wa Kupunguza Taka za Plastiki wa miaka mitano kuanzia mwaka 2026 hadi 2031, ukiwa na lengo la kuimarisha usimamizi wa mazingira na kupunguza athari za taka katika maeneo ya fukwe, mito, mifereji ya maji, barabara na maeneo mengine ya umma.
Kwa mujibu wa mpango huo ambao utatekelezwa na Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Taasisi ya FORUM CC na IUCN unatarajia kufikia asilimia 90 ya ukusanyaji na udhibiti wa taka za plastiki ifikapo mwaka 2029 kupitia kuimarisha mifumo ya ukusanyaji taka, kuongeza uhamasishaji kwa wananchi na kushirikisha wadau mbalimbali katika shughuli za usimamizi wa mazingira.
Akizungumza katika kikao cha kuidhinisha mpango huo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema Kinondoni imepiga hatua kubwa katika usimamizi wa mazingira na usafi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za taka za plastiki, kuimarisha utekelezaji wa sheria za mazingira na kuongeza ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuhakikisha malengo ya mpango huo yanafikiwa.
.hmwinyi