26/05/2026
“HAFLA YA UTIAJI SAINI KATI YA TACAIDS NA NMB FOUNDATION “
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania-TACAIDS imeingia makubaliano pamoja na NMB Foundation kwa lengo la kuunganisha jitihada za kiafya na kifedha kwa walengwa wa Mradi wa Timiza malengo.
Zoezi hilo limefanyika tarehe 26 Mei, 2026 jijini Dodoma ili kufikia malengo ya pamoja kuwasaidia Wasichana balehe na wanawake vijana kuanzia miaka10-24 ambao ni wanufaika wa mradi huo.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania- TACAIDS, Dkt. Adam Mrisho amesema makubaliano hayo yanalenga kuwawezesha Wasichana balehe na wanawake vijana kujikwamua kiuchumi ili Kuwatoa katika hatari ya kupata mambukizi ya VVU (Virusi Vya UKIMWI)
“Umuhimu wa mradi huu ni kuwawezesha vijana hasa wasichana balehe kujikwamua kiuchumi ili kuwatoa katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi ya VVU.
Aidha, Dkt. Mrisho ametoa shukrani kwa NMB Foundation kwa ushirikiano wao Kwani utakua mfano kwa Sekta Binafsi na Sekta za umma kwa kuonesha namna umoja huo unavyoweza kuleta matokeo chanya katika maisha ya vijana na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NMB Foundation Bw. Nelson Karumuna amesema umoja huu ni kwa ajili ya kuwapatia walengwa elimu ya afya na stadi za maisha ili kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuweza kupunguza utegemezi na uchochezi unaoweza kupelekea hatari ya kupata Maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Hadi kufikia makubaliano haya Mradi wa Timiza Malengo umeweza kuwafikia walengwa takribani laki mbili na Ishirini katika Mikoa 10 ukilenga kutoa elimu ya Afya na stadi za maisha ili kuongeza uelewa juu ya VVU na UKIMWI ikiwemo elimu ya Kinga, Matibabu na Matunzo.