15/08/2026
KAMATI YA BUNGE YAISHAURI SERIKALI KUIONGEZA WATAALAM OSHA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeishauri Serikali kuiongezea wataalam Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ili Taasisi hiyo iweze kuimarisha afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi nchini.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Chakoma, Bungeni Jijini Dodoma (Agosti 12, 2026), alipokuwa akifungua kikao cha Kamati kilicholenga kupitia taarifa ya utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Sura Namba 297, Toleo ya 2023 ikiangazia mwenendo wa usajili wa maeneo ya kazi pamoja na utoaji wa elimu ya usalama na afya mahali pa kazi kwa umma kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Taarifa hiyo iliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu ambaye aliambatana na wataalam katika Ofisi yake akiwemo Katibu Mkuu, Bi. Mary Maganga na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Waziri Sangu mbele ya Kamati hiyo, kwa mwaka fedha 2025/2026, OSHA imesajili maeneo ya kazi 16,813 na kutoa mafunzo ya usalama na afya kwa wadau wapatao 45,089 idadi ambayo ni zaidi ya lengo ya kuwafikia wadau 40,000.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za wajumbe wa Kamati, Mtendaji Mkuu wa OSHA amesema maeneo ya kazi yanayosajiliwa na OSHA yanapaswa kukidhi vigezo vilivyowekwa kikiwemo kigezo cha uwepo wa pande mbili zinazotegemeana ambazo ni mwajiri na mwajiriwa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Chakoma, alipokuwa akifanya majumuisho ya michango ya Wajumbe wa Kamati, ameishauri Serikali kuiongezea Taasisi ya OSHA watumishi ili kuiwezesha kutekelezaja majukumu yake ipasavyo kutokana na watumishi 376 waliopo kutokidhi mahitaji ya watendaji wa shughuli za msingi za Taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amesema serikali imejipanga kuendelea kuhamasisha uzingatiaji wa taratibu zote muhimu za usalama na afya kwa waajiri na wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi.