07/09/2026
TPDC 2026 ||
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), limezindua rasmi TPDC Marathon 2026, kampeni inayolenga kukusanya zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuchangia matibabu na upasuaji wa moyo kwa watoto 100 wanaozaliwa na ugonjwa wa moyo nchini.
Uzinduzi huo umefanyika leo katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Johari Rotana, Dar es Salaam, ambapo Kaimu Mtendaji Mkuu wa TPDC, Ndugu Derick Moshi, na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Richard Kisenge, wameeleza umuhimu wa kampeni hiyo katika kusaidia watoto wenye changamoto za moyo na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi.
TPDC Marathon 2026 yenye kaulimbiu “Hatua Yako, Okoa Maisha” inatarajiwa kufanyika tarehe 21 Novemba 2026, ikijumuisha mbio za kilomita 5, 10 na 21. Kupitia mbio hizo, TPDC na JKCI zinawalenga wadau mbalimbali, wakiwemo wananchi, sekta ya nishati na uchumi, taasisi za afya, wadau wa maendeleo na jumuiya za kidiplomasia, kushiriki katika kampeni hiyo ya kuokoa maisha.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Ndugu Derick Moshi amesema kampeni hiyo ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha watoto wenye changamoto za moyo wanapata huduma muhimu za afya, huku akisisitiza kuwa kila hatua na kila mchango ni sehemu ya juhudi za kuokoa maisha na kuwapatia watoto hao matumaini ya kuendelea na maisha yao.