19/06/2025
EPZA yaalika wawekezaji wa Madini kutumia huduma zake.
Mamlaka ya EPZ imeshiriki katika Jukwa la Madini Tanzania lililofanyika jijini Mwanza kati ya Tarehe 15-16 Juni 2025.
Jukwaa hili lilioandaliwa na Wizara ya Madini lilihusisha wadau wa Madini Tanzania nzima zaidi ya 400 wakiwemo wachimbaji wadogo, kati na wakubwa, pia limehusisha wasindikaji wa madini katika ngazi mbalimbali. Pamoja na washiriki hao, viongozi mbalimbali walikuwemo ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wafanyabiashara na Wananchi wa Kawaida.
Akizungumza katika kilele cha jukwaa hilo mgeni rasmi Mhe. Anthony Mavunde (MB) aliwapongeza wadau wa madini na kuwajulisha kuwa mpaka sasa Serikali imekwisha ingiza pato la zaidi ya Bilioni 900, na kufikia mwisho wa mwaka huu mategeo ni kuingiza zaidi ya Trilioni 1.
Aidha katika jukwaa hilo, EPZA ilipata fursa ya kutoa wasilisho ambapo miongoni mwa mambo yaliyowasilishwa ni pamoja na kuonyesha fursa mbalimbali za uwekezaji pamoja na vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ambavyo wadau hao wanaweza kuvipata endapo watatumia leseni za EPZA.
Vivutio hivyo ni Sehemu ya hamasa ambayo Serikali inaitoa ili kuhakikisha kuwa gharama za uzalishaji katika viwanda vya ndani zinashuka ili kusaidia viwanda kuongeza ushindani katika soko la dunia na hivyo kupelekea kuchochea kukua kwa sekta ya Viwanda nchini.
Pamoja na mambo mengine, EPZA imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano maalum kwa ajili ya wadau wa mbalimbali ili kuendelea kutimiza malengo ya nchi katika kufikia Tanzania ya Viwanda.