Bank of Tanzania

Bank of Tanzania This is the official page of the Bank of Tanzania

SERIKALI YAJIVUNIA MCHANGO WA TBA KATIKA KUSTAWISHA SEKTA YA FEDHAMakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleima...
05/09/2026

SERIKALI YAJIVUNIA MCHANGO WA TBA KATIKA KUSTAWISHA SEKTA YA FEDHA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali inajivunia mchango wa sekta ya kibenki katika kustawisha sekta ya fedha, ambayo ni nguzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Mhe. Hemed aliyasema hayo alipohutubia katika hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), iliyofanyika tarehe 4 Septemba 2026, Unguja, Zanzibar.

“Leo tunapoadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TBA, tunajivunia sekta ya kibenki ambayo imekuwa muhimu katika ustawi wa sekta ya fedha na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla,” alisema.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho, Tanzania imepitia mageuzi makubwa katika sekta ya kibenki, ambapo huduma za kibenki zimeondokana na utegemezi wa matawi na huduma za ana kwa ana na kuelekea kwenye mifumo ya kidijitali inayounganisha benki, simu za mkononi na mifumo mbalimbali ya malipo, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi.

“Hatua hiyo imechangia kuleta matokeo chanya, ambapo mamilioni ya Watanzania wameweza kupata huduma za kifedha, mitaji ya biashara, fursa za kuwekeza na kuweka akiba, pamoja na kuchochea uundaji wa ajira na shughuli za uzalishaji, hivyo kuchangia katika kustawisha uchumi wetu,” alisisitiza Mhe. Hemed.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Rahma Mahfoudh, alisema kupitia mabenki ambayo ni wanachama wake, Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) umechangia katika kuelekeza rasilimali za fedha kwenye shughuli za uzalishaji, biashara, kilimo, viwanda, makazi, miundombinu na miradi ya kimkakati ya Taifa.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwezi Julai 2026, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 28.1 kwa mwaka ulioishia Juni 2026. Ukuaji huo umeendelea kusaidia shughuli za uzalishaji na uwekezaji, na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi na uundaji wa ajira nchini.

Aliongeza kuwa sekta ya fedha inatarajiwa kuwa mhimili muhimu katika kuchochea uwekezaji, uzalishaji na ukuaji wa uchumi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Dira hiyo inalenga kuijenga Tanzania yenye uchumi wa takribani Dola za Marekani trilioni moja. Katika mazingira haya, sekta ya fedha haitakuwa mtazamaji, bali mshirika muhimu katika utekelezaji wa Dira hiyo,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania, Bw. Theobald Sabi, alisema hadi mwisho wa mwaka 2025, jumla ya rasilimali za sekta ya benki zilifikia takribani shilingi trilioni 79.4, na kuongezeka hadi takribani shilingi trilioni 84.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026. Katika kipindi hicho, mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kukua kwa takribani asilimia 23.

“Haya ni mafanikio yanayoonesha sekta iliyo imara, inayokua na yenye uwezo mkubwa zaidi wa kuchangia maendeleo ya Taifa letu,” alisema.

Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) ulianzishwa mwaka 1995 wakati Tanzania ikitekeleza mageuzi makubwa ya sekta ya fedha yaliyolenga kuongeza ushindani, kuhamasisha uwekezaji binafsi, kukuza ubunifu na kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha.

04/09/2026
Benki Kuu ya Tanzania kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huuza Dhamana za Serikali za muda mrefu ...
01/09/2026

Benki Kuu ya Tanzania kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huuza Dhamana za Serikali za muda mrefu (Hati fungani) na dhamana za Serikali za muda mfupi (“Treasury bills”) ikiwa ni njia ya Serikali kukopa fedha kutoka kwenye Soko lake la ndani ambapo mnunuzi anaweza kuwa taasisi, vikundi, benki, mtu binafsi n.k.

Dhamana Serikali za muda mrefu ni zile ambazo muda wake wa kuiva unazidi mwaka mmoja. Dhamana hizi huuzwa kwenye soko la awali kwa njia ya ushindani na njia isiyo ya ushindani kupitia minada inayoendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania na baada ya hapo uuzaji wa dhamana za Serikali huuzwa kwenye upili yaani Soko la hisa la Dar es Salaam.

Mwekezaji atanunua Hati fungani kupitia kwa Mawakala ambao ni benki zote za biashara zilizosajiliwa na kupatiwa leseni ya biashara na benki na Benki Kuu ya Tanzania au Mawakala wa soko la Hisa la Dar-es- Salaam waliopatiwa leseni na kusimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana.

Kiwango cha kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali za muda mrefu (Hatifungani) ni kuanzia kiwango cha shilingi 1,000,000.00.

Ili uweze kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali, ni lazima kufungua akaunti maalum ya uwekezaji inayoitwa “Central Depository System Account” – (CDS). Akaunti hii ni tofauti na akaunti ya akiba kwa kuwa inatumika kutunza kumbukumbu na taarifa zote za uwekezaji. Unaweza kufungua akaunti hii kupitia Benki za Biashara au Mawakala.

Kufungua akaunti hii hakuna gharama yoyote, na mwekezaji atatakiwa kuwasilisha nyaraka za utambulisho k**a vile kitambulisho cha taifa (NIDA), namba ya mlipa kodi (TIN), pamoja na picha mbili ndogo za pasipoti.

Wawekezaji wa dhamana za Serikali za muda mrefu hupata malipo ya faida (coupon) mara mbili kwa mwaka, na Benki Kuu ya Tanzania hulipa coupon moja kwa moja kupitia akaunti za benki k**a zilivyoainishwa nakila mwekezaji.

BoT YAONYA DHIDI YA UKOPESHAJI HOLELA NA UPATUBenki Kuu ya Tanzania (BoT) imewaonya wananchi, wakiwemo wasanii na waigiz...
31/08/2026

BoT YAONYA DHIDI YA UKOPESHAJI HOLELA NA UPATU

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewaonya wananchi, wakiwemo wasanii na waigizaji, kujiepusha na kufanya biashara ya ukopeshaji fedha au ukusanyaji wa amana kutoka kwa wananchi kupitia mfumo wa “upatu” au vikundi vingine visivyosajiliwa na mamlaka husika.

Onyo hilo limetolewa leo, tarehe 31 Agosti 2025, katika semina iliyoandaliwa na BoT kwa wasanii wa muziki na waigizaji, ikiwa na lengo la kuwajengea uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya fedha, pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa katika kuendesha shughuli za kifedha.

Akifungua semina hiyo iliyofanyika Benki Kuu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Missango, alisema wasanii ni kundi muhimu kupata elimu hiyo kutokana na ushawishi mkubwa walionao katika jamii.

Alisema ushawishi huo unawapa wasanii nafasi muhimu ya kuwaelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uchumi na fedha, hivyo ni muhimu kuwa na uelewa sahihi ili waweze kutoa taarifa sahihi kwa jamii.

Akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, 2018, Mkaguzi wa Mabenki wa BoT, Bw. Joseph Lubava, alisema kwa mujibu wa Sheria hiyo, mtu au taasisi inayofanya biashara ya huduma ndogo za fedha bila kuwa na leseni halali kutoka BoT anatenda kosa la jinai.

Alisisitiza kuwa mkiukaji anaweza kukabiliwa na faini ya kati ya Shilingi milioni 20 hadi milioni 100 au kifungo cha kati ya miaka miwili hadi mitano jela, pamoja na adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria.

Aidha, alieleza kuwa pamoja na adhabu za jinai, BoT inaweza kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya wakiukaji, ikiwa ni pamoja na kufunga shughuli zinazofanyika kinyume cha sheria, kutaifisha mali zinazohusiana na kosa na kuorodhesha jina la mkiukaji kwa umma.

Mbali na masuala ya ukopeshaji na upatu, semina hiyo pia ilitoa elimu kuhusu utunzaji sahihi wa noti za Tanzania, ikiwemo umuhimu wa wananchi kuzitunza noti katika hali nzuri ili ziendelee kutumika kwa ufanisi katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Bw. Edward Buganga, ameishukuru BoT kwa kutoa elimu hiyo kwa wasanii, ambapo amewasihi kutumia elimu waliyoipata na kuwa mabalozi wazuri wa BoT kwa kuifikisha elimu hiyo kwa jamii, hususan katika maeneo wanayofanya shughuli zao.

BoT imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii kuhusu masuala ya fedha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi na kuhakikisha shughuli za kifedha zinafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

BoT YAIKABIDHI HESLB  URATIBU ZOEZI LA UPATIKANAJI WA WANUFAIKA WA MFUKO WA MWL. JULIUS NYERERE BENKI Kuu ya Tanzania (B...
28/08/2026

BoT YAIKABIDHI HESLB URATIBU ZOEZI LA UPATIKANAJI WA WANUFAIKA WA MFUKO WA MWL. JULIUS NYERERE

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeikabidhi Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jukumu la kusimamia mchakato wa maombi na uteuzi wa wanufaika wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Mwalimu Nyerere Memorial Scholarship Fund), hatua inayolenga kuongeza uwazi, usawa na ufanisi katika utoaji wa ufadhili kwa wanufaika wa elimu ya juu nchini.

Uamuzi huo umeanza kutumika katika udahili wa mwaka wa masomo 2026/27 baada ya Bodi ya Usimamizi wa Mfuko huo kuridhia kutumia mifumo ya HESLB katika mchakato wa kutangaza, kupokea na kuchakata maombi ya wanafunzi wanaostahili kupata ufadhili.

Hayo yamesemwa leo Agosti 28,2026 jijini Dar es Salaam na Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba wakati akizindua Mwongozo Mpya wa Utoaji Ufadhili kwa Wanafunzi wanaonufaika na Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Gavana Tutuba amesema, uamuzi huo ulifikiwa na Bodi ya Mfuko katika kikao chake kilichofanyika Mei,mwaka huu, baada ya kubaini umuhimu wa kutumia mifumo iliyopo serikalini ili kurahisisha mchakato wa kuwapata wanafunzi wenye sifa.

Amesema hapo awali, tangu mfuko huo ulipoanzishwa mwaka 2009, nafasi za ufadhili zilitangazwa kupitia vyombo vya habari, vikiwamo televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii, ambapo wanafunzi wenye sifa waliwasilisha maombi yao na kuchambuliwa na timu ya wataalamu wa BoT.

“Tumekubaliana sasa kutumia mifumo inayoratibiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Mfumo huo una uwezo wa kutumia taarifa za ufaulu kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), hivyo kutuwezesha kupata wanafunzi wenye sifa kwa utaratibu wenye ufanisi zaidi,” amesema Gavana Tutuba.

Amesema,mabadiliko hayo yanaendana na msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa mifumo ya Serikali kusomana ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Gavana huyo, badala ya kuendelea na utaratibu wa kutangaza nafasi na kusubiri maombi, HESLB itaweza kutumia mifumo yake iliyopo kuchakata taarifa za wanafunzi na kubaini wanaokidhi vigezo vya ufadhili.

“Kwa kuwa mfumo wa Bodi ya Mikopo tayari unachakata taarifa za wanafunzi na kubaini wanaostahili kupata mikopo, tumeona ni jambo jema kutumia utaratibu huo huo katika kupata wanufaika wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere,” amesema

Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulianzishwa Oktoba 12, 2009 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuenzi mchango wa Baba wa Taifa katika kuendeleza elimu na rasilimali watu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt.Bill Kiwia amesema, jukumu la kusimamia mchakato wa ufadhili huo ni heshima kubwa kwa taasisi hiyo na ni ishara ya imani iliyowekwa na BoT katika uwezo wa HESLB.

Dkt.Kiwia amesema, ushirikiano huo unaonesha namna taasisi za Serikali zinavyoweza kutumia mifumo na uwezo wao kwa pamoja ili kuboresha huduma kwa Watanzania.

“Leo historia inaandikwa. Bodi ya Mikopo imekabidhiwa jukumu la kutangaza na kupokea maombi ya ufadhili kwa ajili ya vijana wetu wa Kitanzania,”amesema.

Amesema,HESLB imewekeza zaidi ya dola milioni tano katika kujenga na kuimarisha mifumo yake ya kidijitali inayowezesha usimamizi wa mchakato mzima wa mikopo na ufadhili wa wanafunzi.

Miongoni mwa mifumo hiyo ni Mfumo wa Usimamizi wa Maombi Mtandaoni (OLAMS), unaotumika kupokea na kuchakata maombi ya wanafunzi.

Dkt.Kiwia amesema,mfumo mwingine ni Integrated Loan Management System (ILMS), unaowezesha kufuatilia mwanafunzi kuanzia anapoanza masomo, anapoendelea na masomo hadi anapohitimu na kuanza kurejesha mkopo.

Amesema,HESLB pia imejenga mfumo wa kidijitali wa utoaji fedha kwa wanufaika pamoja na mfumo wa malipo ya marejesho unaounganishwa na Serikali e-Payment Gateway (GePG).

Pia,amesema taasisi hiyo imefikia kiwango cha takribani asilimia 98 cha matumizi ya mifumo isiyohitaji karatasi katika shughuli zake, jambo linalorahisisha utunzaji wa nyaraka na uchakataji wa taarifa.

Dkt.Kiwia amesema,HESLB imewezesha zaidi ya Watanzania milioni moja kupata elimu ya juu kupitia mikopo, huku zaidi ya Shilingi trilioni 9 zikitolewa kwa wanufaika.

Amesema,bodi hiyo pia imeendelea kusimamia programu nyingine za ufadhili, ikiwemo Samia Scholarship ambayo tangu ilipoanzishwa mwaka 2022 imewanufaisha zaidi ya wanafunzi 2,000 katika fani za Sayansi, Tiba, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.

Address

16 Jakaya Kikwete Road
Dodoma
40184

Opening Hours

Monday 08:30 - 12:30
14:30 - 16:30
Tuesday 08:30 - 12:30
14:30 - 16:30
Wednesday 08:30 - 12:30
14:30 - 16:30
Thursday 08:30 - 12:30
14:30 - 16:30
Friday 08:30 - 12:30
14:30 - 16:30

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Bank of Tanzania posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Organization

Send a message to Bank of Tanzania:

Shortcuts

Share