08/06/2026
DODOMA YAKABIDHI MWENGE WA UHURU MOROGORO
-Mradi wa Majisafi Nala miongoni wa miradi iliyozinduliwa na Mwenge.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Heri James amekabidhi rasmi Mwenge wa Uhuru Kitaifa wa mwaka 2026 kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro, baada ya kumaliza mbio zake mkoani Dodoma ambapo ulikagua, uliweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katika mbio hizo mkoani Dodoma, miongoni mwa miradi mikubwa iliyomulikwa na kuzinduliwa ni Mradi wa Majisafi wa Nala, ambao ulizinduliwa rasmi Juni 1, 2026. Mradi huo unatajwa kuwa mkombozi mkubwa wa upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.
Katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Wilayani Gairo, mkoa wa Morogoro, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Bernard Rugayi, imeshiriki kikamilifu tukio hilo muhimu ambalo linaashiria mafanikio makubwa katika usimamizi wa miradi ya kimkakati ya maji mkoani humo.