04/09/2026
DKT. MWIGULU: IFIKAPO 2030 MWANZA–DODOMA KWA SGR
▪︎ Aagiza Wizara ya Fedha na Uchukuzi kuharakisha utekelezaji
▪︎ Aelekeza leseni za madini zisizoendelezwa kufutwa
▪︎ Asisitiza kupunguzwa kwa matumizi yasiyo ya lazima
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi, kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), wakandarasi na taasisi zinazohusika na uhamasishaji wa fedha, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya Reli ya Kisasa (SGR), akilenga kuona ifikapo mwaka 2030 wajumbe kutoka Mwanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa wakisafiri kwa treni kutoka Mwanza hadi Dodoma.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 04, 2026) wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge la 13, Mkutano wa Nne, jijini Dodoma.
“Naziagiza Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi, zikishirikiana na Shirika la Reli, wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga vipande hivi pamoja na wale waliopewa jukumu la kuhamasisha fedha za miradi hiyo, kupambana usiku na mchana,” amesema.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha vipande vya Mwanza–Isaka, Isaka–Tabora, Tabora–Kigoma na Makutupora–Dodoma vinaendelea kutekelezwa kwa kasi.
“Ikiwezekana, ifikapo mwaka 2030, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Mwanza, Mara, Shinyanga, Geita na Kagera waje Dodoma wakiwa wamepanda SGR kutoka Mwanza hadi Dodoma,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameiagiza Wizara ya Madini kuchukua hatua za haraka na kali kwa mujibu wa sheria dhidi ya watu wanaoshikilia leseni nyingi za madini bila kuziendeleza, akieleza kuwa hali hiyo inawanyima Watanzania wengine, hususan vijana na wachimbaji wadogo, fursa ya kufanya shughuli za uchimbaji.
“Mheshimiwa Waziri, futeni leseni hizo kwa mujibu wa sheria na gaweni upya maeneo hayo kwa wawekezaji Watanzania, vijana wa Kitanzania na wachimbaji wadogo,” amesema.
Dkt. Mwigulu amewataka Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, watendaji wa Serikali na halmashauri kuhakikisha wanawasikiliza wananchi, wanatatua kero zao kwa wakati na kutoa mrejesho.
Amesema ziara za viongozi wakuu hazipaswi kuwa mbadala wa utatuzi wa kero za wananchi katika ngazi za kawaida za Serikali.