13/08/2026
KAMATI YA SIASA CCM MKOA YAPONGEZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA ELIMU NA UWEZESHAJI VIJANA LINDI
Na Dawla Muni-Lindi MC
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Lindi, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Alhaj Hassan M. Jarufu, imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Lindi, ikiwemo uwekezaji katika elimu na uwezeshaji wa vijana.
Kamati hiyo imepongeza ujenzi wa Shule ya Msingi Mmongo, Kata ya Rasbura, unaogharimu Shilingi milioni 314 kupitia mpango wa BOOST, ambapo ujenzi wa jengo la utawala na madarasa mawili ya awali umefikia asilimia 97.
Mhe. Jarufu amesema elimu ni msingi wa maendeleo na amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga shule zenye mazingira bora, huku akihimiza mradi huo ukamilike kwa wakati.
Aidha, Katika ziara hiyo Kamati pia imepongeza utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana baada ya kukagua Kikundi cha Youth Garage chenye wanachama watano, kilichopatiwa Shilingi milioni 34.
Mkopo huo umewezesha ununuzi wa vifaa vya ufundi magari, vipuri na mashine za rangi, na tayari umezalisha ajira na fursa za mafunzo kwa vijana. Kikundi hicho kimerejesha Shilingi laki saba hadi sasa.