31/08/2026
MEMKWA na SEQUIP mkombozi wa watoto na watu wazima wenye kiu ya elimu.
Na. Lina Sanga
Jamii imetakiwa kutambua umuhimu wa elimu na kutakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuhakikisha watoto na watu wazima waliokosa elimu katika mfumo rasmi wanapata elimu kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliyoikosa (MEMKWA) na Mpango wa uboreshaji wa elimu YA sekondari (SEQUIP),inayomwezesha mwanafunzi mwenye umri wa miaka 9 hadi 22 kusoma kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.
Wito huo umetolewa leo na Mhe. Robert Shejamabu, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako, katika maadhimisho ya juma la elimu ya watu wazima, yaliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya zamani ya Kijiji cha Ikelu.
Mhe. Shejamabu amesema kuwa, licha ya mpango huo wa Serikali kuwawezesha wananchi kielimu ipo haja ya jamii kutambua umuhimu wa elimu licha ya ajira za Serikali kutotosheleza idadi ya wasomi Nchini,kwani elimu inaongeza ufahamu na kwa sasa kupitia shule za amali mhitimu anaweza kujiajiri na kunufaika kupitia elimu aliyonayo.
Ametoa wito kwa vijana kutochagua kazi baada ya kuhitimu masomo na kuwataka kujishughulisha kwa kazi mbalimbali hata ambazo ni tofauti na taaluma walizonazo k**a kilimo na ujasiriamali,wakati wakisubiri ajira rasmi na kuwataka wazazi watambue kuwa, wanasomesha watoto ili wapate ufahamu na kujiongezea maarifa na sio kuajiriwa pekee kwani dunia ya leo inahitaji watu wenye ujuzi wa vitu mbalimbali.
“Ili Halmashauri yetu iendelee na Nchi yetu iendelee tunahitaji vijana wetu wasome na wazazi tuwe na ufahamu wa elimu, angalau elimu ya kusoma,kuandika,na kuhesabu tuwe nayo,hata k**a umri umeenda tuwekeze kwa watoto”alisema Mhe. Shejamabu.
Amewataka wanafunzi kuishika elimu na wazazi kuwapeleka watoto shuleni ili kutopata lawama pindi watoto wakiwa watu wazima pamoja na kutowaficha ndani watoto wenye mahitaji maalum kwani elimu ni haki ya kila mtoto.
Pia, ametoa wito kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbalimbali pamoja na mitambo ya kilimo kujitangaza kupitia vyombo vya habari,ili wananchi waliopo ndani na nje ya Makambako wawatambue na kufika kwenye viwanda vyao kujifunza ufundi na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.
Frank Filangali, Mmiliki na fundi wa mitambo ya kilimo wa kiwanda cha Tuonane fabrication workshop kilichopo Mtaa wa Majengo,Halmashauri ya Mji Makambako ameishukuru ofisi ya Mkurugenzi kwa kuandaa maonyesho ya bidhaa katika maadhimisho hayo na kutoa rai kwa wananchi wanaotaka kujifunza ufundi wa zana za kilimo kufika katika kiwanda chake ili waweze kupata zana hizo pamoja na maarifa.
Naye,Adriano Mdenye mwanafunzi katika shule ya sekondari Makambako,taasisi ya elimu ya watu wazima ameishukuru Serikali kwa kutoa fursa kwa wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali, na kuwataka wazazi kutowakatia tamaa watoto wao ambao walikatiza masomo kwani inawezekana kuendelea na masomo na kutimiza malengo yao.