30/05/2026
NAIBU WAZIRI WA ARDHI AFANYA ZIARA MOROGORO DC, ASISITIZA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI KWA KUZINGATIA SHERIA
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, leo Jumamosi Mei 30, 2026, amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za ardhi zinazowakabili wananchi.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mmuya alifanya mikutano ya hadhara katika Kijiji cha Mbwade kilichopo Kata ya Bwakila Chini na Kijiji cha Msonge kilichopo Kata ya Mvuha, ambapo alipokea na kujadili changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya ardhi.
Naibu Waziri huyo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, M***a Kilakala, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini , Zuberi Yahaya Mfaume.
Akizungumza na wananchi katika mikutano hiyo, Mheshimiwa Mmuya alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Hata hivyo, aliwataka wawekezaji kuhakikisha wanazingatia na kuheshimu makubaliano wanayoingia na wananchi ili kuepusha migogoro inayoweza kuathiri amani na maendeleo ya maeneo husika.
Aidha, aliwasihi wakulima na wafugaji kutumia njia za kisheria katika kutatua migogoro yao badala ya kujichukulia sheria mkononi, akisisitiza kuwa kufuata taratibu zilizowekwa kutasaidia kudumisha amani na kuimarisha ushirikiano kati ya makundi mbalimbali ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mmuya alimpongeza Mbunge wa Morogoro Kusini, Mheshimiwa Zuberi Yahaya Mfaume, kwa juhudi zake za kuwasilisha na kusimamia hoja mbalimbali zinazolenga kutatua kero za wananchi na kuharakisha maendeleo katika jimbo hilo.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za awamu ya sita kuendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa karibu, hususan katika sekta ya ardhi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.