07/08/2026
MNYAMAPORI ANAJUA MPAKA WA HIFADHI?!
📍 Nini kifanyike?
✍️ Na Beatus Maganja
“Njooni muwaondoe tembo wenu, tayari wameshavamia mashamba yetu” Ni kauli ambayo mhifadhi anaweza kukutana nayo baada ya tembo kutoka katika eneo la hifadhi na kuingia mashambani, wakati mwingine akila au kuharibu mazao.
Kwa mwananchi aliyepoteza mazao aliyoyategemea kwa chakula au kipato, hasira na maumivu yake yanaeleweka na kwakweli inaumiza sana. Lakini katikati ya hali hiyo kuna swali ambalo ni muhimu sana kujiuliza..Je, tembo anajua mpaka wa hifadhi?. Na huu ndio msingi wa makala hii.
Sisi binadamu tuna ramani. Tuna alama za mipaka, vigingi, barabara, vijiji, kata, wilaya, mikoa na hata mipaka ya nchi. Tunaweza kusema, “Kuanzia hapa ni hifadhi, na kuanzia pale ni ardhi ya kijiji.” Lakini kwa tembo au mnyamapori mwingine, dunia yake haisomeki kwa namna hiyo. Mnyama hawezi kusoma bango lililoandikwa “Mwisho wa Hifadhi”, wala hawezi kujua kwamba hatua chache mbele yake amevuka mpaka uliowekwa na binadamu.
Kwa mnyamapori, kinachoongoza mienendo yake zaidi ni mahitaji yake ya msingi katika maisha. Anatafuta maji, chakula, mwenza, eneo salama la kuzaa au njia ya kuelekea kwenye mazingira yanayokidhi mahitaji yake. Baadhi ya wanyamapori hutumia maeneo makubwa na wanaweza kusafiri umbali mrefu kulingana na upatikanaji wa maji, chakula, misimu na hali ya mazingira. Kwao, mfumo ikolojia unaweza kuwa muhimu zaidi kuliko mstari wa mpaka tuliochora kwenye ramani.
Ndiyo maana tunapozungumzia uhifadhi, hatuwezi kuzungumzia hifadhi peke yake. Lazima tuzungumzie pia mapito ya wanyamapori (wildlife corridors), maeneo ya mtawanyiko (dispersal areas) na maeneo yanayounganisha mifumo mbalimbali ya ikolojia. Maeneo haya yanaweza kuwa muhimu kwa wanyama kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta rasilimali muhimu kwa maisha yao. Yakizibwa kabisa na shughuli za kibinadamu, uwezekano wa kukutana kwa binadamu na wanyamapori unaweza kuongezeka.
Kwa upande mwingine. hebu tufikirie jambo hili Kwa pamoja. Njia ambayo leo tunaiita shamba, kijiji au makazi ya watu inaweza kuwa sehemu ya eneo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa likitumiwa na wanyamapori kupita. Kadiri idadi ya watu inavyoongezeka na matumizi ya ardhi kubadilika, maeneo ya makazi, kilimo, mifugo na miundombinu yanaweza kusogea karibu zaidi na maeneo wanayotumia wanyamapori. Hapo ndipo wakati mwingine tunapoanza kusema, “Wanyama wamekuja kwetu.” Lakini swali la kutafakari ni hili...Je, katika baadhi ya maeneo, ni wanyamapori waliotufuata, au matumizi yetu ya ardhi ndiyo yaliyokutana na njia zao za muda mrefu?.
Hapa ndipo Mamlaka husika zimekuwa zikifanya kila ziwezavyo kuhakikisha zinatafuta suluhu ya kudumu ya jambo hili, ili kuhakikisha mwananchi anaendelea kuwa salama dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao, na wanyamapori pia k**a rasilimali muhimu ya Taifa kuendelea kuwepo Kwa manufaa ya kizazi chetu na vizazi vijavyo.
Kwahiyo, tunapomuona tembo nje ya hifadhi, ni vyema tusifanye haraka kuhitimisha kwamba “amekosea njia.” Huenda kwa mtazamo wetu yuko nje ya mpaka, lakini kwa mtazamo wa ikolojia anaweza kuwa anafuata maji, chakula au njia ambayo vizazi vya wanyama wa aina yake vimeitumia kwa muda mrefu. Changamoto yetu sisi binadamu ni kutafuta namna ambayo mahitaji ya maendeleo, usalama wa wananchi na mahitaji ya wanyamapori yanaweza kusimamiwa kwa uwiano.
Mwisho wa yote, mnyamapori hajui mpaka wa hifadhi kwa namna tunavyoujua sisi. Hajui kijiji kinaanzia wapi wala hifadhi inaishia wapi. Lakini sisi tunajua. Tuna sayansi, teknolojia, sheria na uwezo wa kupanga matumizi ya ardhi. Hivyo jukumu kubwa zaidi liko kwetu kutumia maarifa hayo kuhakikisha binadamu anaishi kwa usalama huku wanyamapori na makazi yao yakiendelea kuhifadhiwa.
Kwasababu swali kubwa si tu, “Kwa nini mnyama ametoka hifadhini?” bali pia tunapaswa kujiuliza..Je, tumemwachia njia ya kwenda anapohitaji kwenda? Kwa maana uhifadhi ni zaidi ya kulinda mnyama ndani ya mpaka pamoja na kuelewa maisha yake hata pale yanapovuka mpaka.