04/08/2026
MWANG’ONDA AWAPONGEZA WANANCHI WA NTAGACHA, TARIME
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 Ndugu Wazo Michael Mwang’onda leo amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Ntagacha kwa kujitolea shilingi 31,863,800.00 kwa ajili ya kujenga nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Ntagacha, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi katika ujenzi huo, Ndugu Mwang’onda amewapongeza wananchi kwa juhudi zao na kuongeza kuwa kwa kutambua juhudi hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imeahidi kuongeza shilingi milioni 10 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo ambayo kwa sasa ujenzi wake upo katika hatua ya kupiga lipu.
“Ninawapongeza sana wananchi kwa juhudi mlizozifanya katika kuanzisha ujenzi wa nyumba hii hadi hatua ilipofikia, Mwenge wa Uhuru unatambua juhudi zenu za kujiletea maendeleo katika kijiji chenu” amesema Ndugu Mwang’onda.
Ndugu Mwang’onda amewataka wahandisi wa Halmashauri kusimamia vizuri ujenzi unaofanywa kwa nguvu za wananchi katika maeneo yao ili kupata majengo bora yanayoakisi gharama iliyotumika na kwa kuwa majengo hayo baada ya kukamilika ni mali ya Serikali hivyo yanapaswa kuzingatia michoro na viwango vya utekelezaji wa mradi wa Serikali.
Aidha, akizungumza katika maeneo tofauti tofauti, Ndugu Mwang’onda amewahamasisha wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kulinda amani, utulivu na mshik**ano wa kitaifa katika maeneo yao na kuwaeleza kuwa bila ya amani hamna maendeleo ya mtu binafsi, taasisi wala nchi yanayoweza kufanyika.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime umetembelea miradi ya maendeleo saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 10 ambayo imejengwa kwa fedha za wananchi, Serikali Kuu, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na wahisani wa maendeleo.
Mwenge wa Uhuru umetembelea kikundi cha vijana Nyamongo Construction Group na ukiwa hapo umepokea taarifa, kukagua mradi na umezindua gari la mizigo la kikundi hicho; umezindua Hoteli ya Silver Spring, umezindua madarasa mawili katika shule ya Msingi Matongo, umezindua daraja la Nyangoto-Matongo na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Genkuru na Msege miradi yote ikiwa katika eneo la Nyamongo.
Aidha, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi wa jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Magoto na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa nyumba ya watumishi wa Shule ya Msingi Ntagacha.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Shule ya Sekondari ya Matongo umetembelea na kuzindua Klabu ya Mazingira na kupanda miti ya matunda na kutembelea Klabu ya Rushwa katika Shule ya Sekondari ya Matongo.
Mkesha wa Mwenge wa Uhuru unaendelea katika Uwanja wa Mwenge Sirari, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kesho Mwenge wa Uhuru utakabidhiwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kuendelea na mbio zake.