10/11/2023
BODI YA TAIFA YA MAJI YATEMBELEA CHANZO CHA MAJI YA ZIWA VICTORIA- IHELELE
Wajumbe wa Bodi ya Maji ya Taifa wamefanya ziara ya siku moja ya kutembelea chanzo cha Maji ya Ziwa Victoria- Ihelele kilichopo katika kitongoji cha Ihelele, Kijiji cha Nyang’homango, Kata ya Ilujamate, Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza.
Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Mbogo Futakamba ambae alifuatana na wajumbe wa Bodi hiyo pamoja na wataalam kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama- Shinyanga (KASHWASA).
Lengo kuu la ziara hiyo ni kujionea uhifadhi wa chanzo cha maji cha Ziwa Victoria - Ihelele na shughuli za uzalishaji maji pamoja na uendeshaji wa mradi huo.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria Dkt. Renatus Shinhu amesema, chanzo hicho ni kati ya miradi mikubwa ya kitaifa ambacho hutoa maji Ziwa Victoria kwa ajili ya kusambaza kwa wananchi ili kuwapatia maji safi na salama.
Chanzo hicho kinatumiwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (KASHWASA) na KASHWASA wanazalisha maji kina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 63 kwa siku.
Dkt. Shinhu ameongeza kuwa, mradi huo unatoa huduma ya maji kwa watu 1,969,255 katika miji ya Kahama, Shinyanga, Nzega, na Tabora. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi ya watu milioni mbili baada ya kupanuliwa kwenda katika miji ya Urambo, Igunga na Shelui.
Katika jitihada za kutunza na kuhifadhi chanzo hicho, Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imefanya uhamasishaji na kutoa elimu kwa vijiji 18 vinavyozunguka chanzo, kusimika vigingi 4700 kwa upande wa wilaya ya Misungwi kwa umbali wa Kilomita 197 na upande wa Wilaya ya
Nyang’hwale kwa umbali wa Kilomita 85,` kupanda miche ya miti 25,000 kwenye ekari 120 na kusimika mabango 32 ya katazo pamoja na kuunda jumuiya tatu (3) za watumia maji ambazo ni (i) Jumuia ya Watumia Maji Ihelele (ii) Jumuiya ya Watumia Maji Ligembe juu na (iii) Jumuia ya Watumia Maji Ligembe chini.