30/08/2026
MILIONI 32.8 ZACHANGISHWA UKARABATI WA SHULE YA SEKONDARI MBEYELA
Jumla ya Sh. 32,828,500/= zimepatikana katika harambee ya kuchangia ukarabati wa majengo ya Shule ya Sekondari Mbeyela, Kata ya Njombe Mjini, Halmashauri ya Mji Njombe.
Katika harambee hiyo iliyofanyika tarehe 29 Agosti 2026, wananchi na wadau mbalimbali walijitokeza kuchangia fedha na vifaa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe, Mhe. Erasto Mpete, amesema lengo la harambee hiyo ni kuimarisha miundombinu ya shule ili kuinua kiwango cha taaluma na kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi pamoja na walimu.
“Maendeleo yanaanza na sisi ndugu wananchi. Niombe tushirikiane kwa pamoja kuchangia harambee ya shule yetu,” amesema Mhe. Mpete.
Mhe. Mpete pia amewahimiza wananchi kutumia fursa ya kilimo cha parachichi kwa kupanda angalau miti mitano kwa kila familia, ili kuongeza kipato na uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Jimmy Ngumbuke amewashukuru wabunge, madiwani,Viongozi wa serikali, wafanyabiashara, wakulima wa parachichi na wananchi wote waliochangia kufanikisha zoezi hilo.
Kwa mujibu wa matokeo ya harambee hiyo, Shilingi 7,893,500 zilipatikana kwa njia ya fedha taslimu, huku Shilingi 11,400,000 zikiwa ni ahadi za fedha na Shilingi 13,535,000 zikiwa ni ahadi za malighafi, hivyo kufikisha jumla ya Shilingi 32,828,500.
Uongozi wa shule umeeleza kuwa zoezi la uchangiaji bado linaendelea, hivyo wananchi na wadau ambao hawakupata nafasi ya kushiriki katika harambee hiyo wanaendelea kupewa fursa ya kuchangia kupitia akaunti ya NMB 60610003749, yenye jina Joseph Mbeyela Secondary, huku wanaochangia wakitakiwa kuwasilisha slip ya malipo kwa uongozi wa shule kwa ajili ya kumbukumbu.