01/09/2026
DC GONDWE AAGIZA KAMATI YA LISHE KUFUATILIA UTEKELEZAJI WA AFUA YA LISHE MASHULENI.
Johnson Soah na Emmanuel Kimu
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, ameagiza Kamati ya Lishe ngazi ya Wilaya kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa afua ya lishe mashuleni ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula.
Mhe. Gondwe ametoa maagizo hayo leo Septemba 1, 2026 wakati akiongea katika Kikao cha Robo ya Nne ya mwaka 2025/2026 kilichofanyika katika ukumbi Chuo cha Maabara Singida.
Amesema ni muhimu kamati hiyo kushirikiana na Maafisa wa Elimu ngazi zote, Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa pamoja na Madiwani kuhakikisha wanafika katika shule zote.
"Nawaagiza Watendaji wa Kata kushirikisha viongozi wengine katika kata zenu kuhamasisha lishe mashuleni. Wakaazi, walezi, Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji pamoja na Maafisa Lishe wote mshirikishwe,". Amesisitiza Mhe. Gondwe.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza Idara ya Afya kutoa elimu kwa akina mama wajawazito kuhusu umuhimu wa kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo yao na kupata ushauri wa wataalamu katika kila hatua ya ukuaji wa mtoto.
Aidha, amewataka wajawazito kuendelea kujifungulia katika vituo vya afya ili kuepuka vifo vinavyoweza kuzuilika, kwani Serikali imewekeza rasilimali za kutosha katika hospitali na vituo vya afya.
Kwa upande wake, Kamati ya Lishe Wilaya ya Singida imesema imepokea maagizo hayo na itaenda kuyatekeleza mara moja.