30/07/2018
Jamii imetakiwa kiwafichua viongozi wanaokiuka maadili
..............
VIJANA wameaswa kushiriki kikamilifu katika kujenga nchi kwa kuibua matendo ya uvunjwaji wa maadili yanayofanywa na baadhi ya Viongozi wa Umma nchini.
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili, Mhe: Asaa Ahmad Rashid amewaeleza Vijana wa Mabaraza ya Vijana Wilaya za Magharibi na Mjini wakati akifungua mkutano wa siku moja uliojadili nafasi ya Vijana katika kuimarisha maadili kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni mjini Unguja.
Mhe: Rashid aliitaja nafasi ya vijana kuwa ni kutoa elimu ya umuhimu wa maadili katika jamii, kuripoti taarifa za ukiukwaji wa maadili na kushirikiana na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kutekeleza majukumu yake.
“Maendeleo ya nchi yanategemea uimara wa vijana na ndio maana tunasema kijana ni nguvu kazi ya taifa. Jamii ikiwa na vijana dhaifu wasioweza kusimamia rasilimali za nchi yao, wasioweza kuwa na uchungu na nchi yao ni wazi kuwa taifa litakuwa katika hatari”. Alifahamisha.
Amewataka vijana kuzitumia nafasi zao vizuri kwa kuhakikisha maadili yanalindwa na kutekelezwa kila mahali ikiwemo katika ngazi ya familia, jamii, taasisi za elimu, taasisi za dini, sehemu za kazi na kila sehemu ambazo wanakutana.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa viongozi pamoja na watumishi wa umma wanatekeleza majukumu ambayo jamii ina uhitaji kwao hivyo ni lazima wazingatie maslahi ya umma na si vyenginezo katika kutekeleza majukumu yao.
Amefahamisha kuwa jamii yoyote ile haiwezi kupiga hatua za kimaendeleo bila ya kuwa na maadili mazuri ambayo huhitaji watu wa kuyaendeleza ili kizazi na kizazi kiweze kurithi.
Akizitaja baadhi ya faida zitakazoweza kupatikana endapo vijana hao na jamii watasimamia maadili ipasavyo kuwa ni kuimarika kwa maendeleo ya nchi, kuzidisha amani, upendo na utulivu, kuondoka kwa dhulma nchini, kuzidisha hali ya umoja na mshik**ano, kujenga uaminifu na uadilifu, kuondoka kwa rushwa na uhujumu uchumi katika jamii.
Kwa upande mwengine, akiyazungumzia matendo ya udhalilishaji nchini, watumishi kutoa siri za wanaowahudumia k**a vile madaktari kutoa siri za wagonjwa, kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na kuongezeka kwa madawa ya kulevya ni athari kubwa zilizopo nchini kutokana na kuacha kufuata maadili.
Aidha, Mwenyekiti wa Tume hiyo akiyazungumzia baadhi ya mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema kuwa kuanzishwa kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar ni jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Rais Dkt. Ali Mohamed Shein katika jitihada za kuimarisha utawala bora nchini.
Naye Katibu wa Tume hiyo Ndugu Kubingwa Mashaka Simba alisema kuwa Tume hiyo itaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia makundi tofauti kwani ni moja katika majukumu ya Tume hiyo kisheria.
Amefahamisha kuwa Tume hiyo itachukua hatua kwa kiongozi yeyeto yule endapo itabainika kuwa kiongozi huyo amekiuka miiko na taratibu za uongozi.
Katika mkutano huo mada mbili ziliwasilishwa ikiwemo Sheria ya Maadili na Umuhimu Wake na Jukumu la Mabaraza ya Vijana Katika Kukuza Maadili ambapo vijana waliweza kupata nafasi ya kuchangia mada hizo.
Wakitoa michango yao mbele ya Tume, vijana hao wameitaka Tume hiyo izidi kuendelea kutoa elimu hiyo hususan kwa viongozi wa umma kwani wamesema kuwa kumekuwepo kwa matumizi mabaya ya vyombo vya Serikali vinavyotumika kwa maslahi binafsi.
Aidha, wameishauri Tume kushughulikia viongozi ambao hawawajali wananchi wao kwa kuwatolea lugha zisizofaa wananchi wao.
Mkutano huo uliwashirikisha wajumbe wa mabaraza ya vijana wa Wilaya za Magharibi, Mjini na wajumbe wa Baraza la Vijana Taifa ambapo elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa mabaraza yote ya Vijana wa Wilaya za Unguja na Pemba.