28/08/2026
WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KAMBI YA BURE YA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MACHO ZANZIBAR
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika Kambi Maalumu ya Uchunguzi na Matibabu ya Macho itakayofanyika kuanzia Agosti 29 hadi Septemba 4, 2026 katika mikoa ya Kaskazini Unguja na Mjini Magharibi, ambapo huduma zote zitatolewa bila malipo.
Wito huo umetolewa leo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Mhandisi Ussy Khamis Debe, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kambi hiyo, inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya macho kwa wananchi.
Alisema kuwa Kambi hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya Zanzibar na Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwa udhamini wa Qatar Charity, ikiwa na lengo la kuwafanyia uchunguzi wa macho wananchi 2,050.
Kwa mujibu wa Mhandisi Debe, wananchi watakaobainika kuwa na matatizo ya macho watapatiwa huduma stahiki kulingana na mahitaji yao, zikiwemo miwani na upasuaji wa macho.
“Kambi hii ni sehemu ya juhudi za kupunguza changamoto za uoni na kuzuia ulemavu wa macho unaoweza kudhibitiwa au kutibiwa,” alisema Mhandisi Debe.
Alisema awamu ya kwanza ya kambi hiyo itafanyika katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kuanzia Agosti 29 hadi 31, 2026 katika Kituo cha Afya Kinduni, huku awamu ya pili ikifanyika Mkoa wa Mjini Magharibi kuanzia Septemba 1 hadi 4, 2026 katika Kituo cha Afya Sebleni.
Alifafanua kuwa katika kambi hiyo, wananchi 400 wanatarajiwa kupatiwa miwani, huku 417 wakitarajiwa kufanyiwa upasuaji wa macho. Wananchi wengine watakaobainika kuwa na matatizo mengine ya macho watapatiwa huduma kulingana na hali zao.
Mhandisi Debe alisema baadhi ya changamoto za macho zinazoweza kusababisha ulemavu hazitokani na hali ya kuzaliwa, bali zinaweza kusababishwa na maradhi au changamoto nyingine za kiafya, hivyo akasisitiza umuhimu wa wananchi kufanya uchunguzi wa macho mapema.
“Uchunguzi wa mapema ni muhimu kwa sababu unasaidia kubaini matatizo ya macho katika hatua za awali na kuwezesha matibabu au udhibiti wa tatizo kabla halijawa kubwa zaidi,” alisema.
Amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Zanzibar ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa asilimia 3.6 ya watu wenye umri wa miaka saba na zaidi Zanzibar waliripoti kuwa na ugumu wa kuona, hali inayofanya tatizo la kuona kuwa miongoni mwa changamoto kubwa za ulemavu zilizoripotiwa.
Mhandisi Debe alisema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya macho, hasa kwa kuzingatia kuwa baadhi ya matatizo ya uoni yanaweza kutibiwa au kudhibitiwa iwapo yatagunduliwa mapema.
Aliwashukuru Qatar Charity kwa udhamini wa programu hiyo na kuitaka jamii kutumia fursa hiyo kwa kufika katika vituo vilivyotengwa ili kupata huduma.
Alisisitiza kuwa, huduma hizo hazitakuwa kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vituo hivyo pekee, bali wananchi kutoka maeneo mengine wenye changamoto za macho wanaruhusiwa kufika kupata huduma.
Aidha, alisema mipango inaendelea kuhakikisha huduma za aina hiyo zinafika pia kwa wananchi wa Pemba ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya ya macho katika Zanzibar.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Qatar Charity nchini Tanzania, Amjad Altahhan, alisema taasisi hiyo imeanzisha na kudhamini kampeni hiyo ikiwa sehemu ya juhudi zake za kijamii za kusaidia wananchi kupata huduma muhimu za afya, hususani huduma za afya ya macho.
Alisema Qatar Charity itashirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili katika kusimamia na kuendesha zoezi hilo ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wenye changamoto za macho wanapata huduma wanazohitaji na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na kutopata matibabu kwa wakati,” alisema.
Naye Mratibu wa Huduma za Afya ya Macho kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Fatma Juma Omar, alisema huduma za uchunguzi na matibabu ya macho zimekuwa zikitolewa mara kwa mara, huku ushirikiano na Qatar Charity ukiwa umeongeza uwezo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Daktari Bingwa wa Maradhi ya Macho kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Johannes Mafwiri, alisema kambi hiyo itatumia mfumo wa huduma ya mkoba, ambapo wataalamu na vifaa vya matibabu husogezwa karibu na wananchi badala ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.
“Mfumo huu utasaidia kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi wanaohitaji uchunguzi na matibabu ya macho,” alisema Dk. Mafwiri.
Alisema kambi hiyo itahusisha wataalamu bingwa na bobezi wa maradhi ya macho, ambao watafanya uchunguzi na kutoa matibabu kulingana na aina na ukubwa wa tatizo la kila mgonjwa.
Dk. Mafwiri aliongeza kuwa katika kambi hiyo, kwa mara ya kwanza, wataalamu watafanya baadhi ya upasuaji wa macho kwa kutumia mfumo wa matundu madogo ndani ya gari maalumu la matibabu.
Alisema teknolojia hiyo inatarajiwa kuwasaidia wagonjwa kupata nafuu kwa haraka na kurejea katika shughuli zao za kila siku kwa muda mfupi zaidi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa huduma hiyo, Dk. Mafwiri aliwasisitiza wananchi wenye changamoto za kuona kutumia fursa hiyo kwa kufika katika vituo vilivyotengwa ili kupata uchunguzi na matibabu bila malipo.
Kambi hiyo inatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za pamoja za Serikali na wadau wa afya katika kuimarisha huduma za macho Zanzibar, kupunguza changamoto za uoni na kuzuia ulemavu wa macho unaoweza kuzuilika au kutibiwa.