03/09/2026
WIZARA ya Afya Zanzibar kupitia Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imefanya mkutano wa kuwasilisha matokeo ya mradi wa ZAN-TOTO, uliolenga kuimarisha matumizi sahihi ya dawa za antibiotiki, hususan kwa watoto.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Maryam Seif Hemed, amesema matumizi sahihi ya antibiotiki ni muhimu katika kulinda afya ya wananchi, huku matumizi yasiyo sahihi yakisababisha madhara kwa afya ya mtu binafsi na kuongeza gharama kwa Serikali.
Amesema matumizi holela ya antibiotiki yanaweza kufanya baadhi ya magonjwa kuchukua muda mrefu kupona, pamoja na kusababisha vijidudu vinavyosababisha magonjwa kuzoea dawa hizo na hivyo kuwa vigumu kutibiwa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa upande wa Zanzibar, Dkt Ndoungou Salla Ba amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha matumizi sahihi ya antibiotiki hasa kwa watoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu katika Taasisi ya Afya Zanzibar ZAHRI, Dkt Mayasa Salum Ali amesema kuwa mradi wa Zan Toto Project umemalizika baada ya kutekeleza kampeni ya kukabiliana na matumizi mabaya na holela ya dawa za antibayotiki Zanzibar.
Amefahamisha kuwa mradi huo ulisaidiwa kutekelezwa na ICARS umetumia takriban shilingi bilioni 1.5 na kutekelezwa katika hospitali tano za Zanzibar, ikiwemo Hospitali ya Mnazi Mmoja na Kivunge kwa Unguja na hospitali tatu za Pemba ambazo ni Kinyasini, Vitongoji na Abdalla Mzee.
Nae Mkuu wa Taasisi ya ICARS Afrika Dkt Titha Dzowela amesema wameshirikiana na Zanzibar katika kuimarisha juhudi za kukabiliana na matumizi yasiyofaa ya dawa za antibayotiki, kupitia mradi wa Zan Toto Project huku mradi huo ukiwezesha kufanyika kwa tafiti na kampeni za uhamasishaji, hususan kwa kuangalia matumizi ya dawa hizo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano dhidi ya usugu wa dawa za antibayotiki.
Kwa upande wa Mratibu wa Mradi wa Zan Toro Project, Muhidin Omar, amesema kuwa mradi huo wa miaka 3 ulitakiwa kutekelezwa kwa kiwango cha 30%, lakini kupitia utekelezaji wake wamefanikiwa kupunguza changamoto zilizokuwa zikikabili huduma hizo kwa 25%.