30/04/2024
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na juhudi za kuyarejesha mashamba yote ya Misitu ya Unguja na Pemba kwa kupanda miti ili kukidhi mahitaji ya wananchi KWA Kuni na miti ya Ujenzi
Akizungumza katika Siku ya Upandaji Miti kitaifa katika Shamba la Misitu Chaani-Masingini kwa niaba ya Waziri wa kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Mkuu wa Wilaya ya kaskazini "A" Othman Ali Maulid amesema hatua hiyo itaondoa tatizo la upatikanaji wa nishati ya kupikia na Miti ya Ujenzi na kupunguza Utegemezi wa Misitu ya asili.
Alisema ni vyema kuongeza juhudi za kupanda miti badala ya kuikata pekee ili lengo linalohitajika liweze kufikiwa.
Aidha amefahamisha kuwa Shamba la Misitu la Chaani-Masigini pamoja na Mashamba mengine ya Misitu ya Dunga-Jendele, Kibele na Unguja Ukuu kwa Upande wa Unguja na Maziwa ng'ombe kwa Pemba yalitangazwa kuwa maeneo ya hifadhi katika gazeti rasmi la Serikali la mwaka 1987 ambapo mashamba hayo yalianzishwa kupitia mradi wa kuendeleza Misitu Zanzibar uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo Finland lengo lake kuu ni uanzishaji wa Mashamba hayo ili kuongeza Uzalishaji wa mazao ya Misitu na kupunguza utegemezi wa Misitu ya Asili
" Shughuli yetu hii ya Upandaji miti hapa leo katika mashamba yaliyotajwa hapo juu na maeneo mengine inaendana na Program ya nchi ya kurejesha urithi wa Kijani Zanzibar kwani Urudishaji wa Mashamba haya Utasaidia kupunguza Utegemezi na Ukataji wa Mikoko na Msitu wa Hifadhi ya Akiba wa Kiwengwa-pongwe kwa ajili ya kuni hususani kwa waanika Madagaa wa Fungu refu na Maeneo mengine na Matumizi ya Bekari" alisema Othman.
Othman Aliongeza kwa kutoa Wito kwa Wakulima endapo mkulima anataka kulima katika maeneo hayo basi alime kwa kufuata maelekezo kwa Wataalamu ili kuendelea kulima huku wakitunza Miti iliyopandwa kwani Atakaebainika ameing'oa miti hiyo Wizara haitowacha kuchukua hatua za kisheria Pamoja na kumuondoa katika eneo hilo.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ali khamis Juma amesema Pamoja na Kuhamasika juu ya Matumizi ya Nishati mbadala ikiwemo gesi na Umeme bado kuna umuhimu wa kuendelezwa Mashamba hayo kwa lengo la awali kutokana na jamii kutumia Nishati za kuni na makaa na Uwepo wa Mashamba ambao utaweza kusaidia kupata huduma hizo.
Hata hivyo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya kilimo itaendelea kutoa elimu juu ya Upandaji wa miti na Uhifadhi wa Misitu ili itowe tija kwa Serikali na Jamii kwa Ujumla.
Nae Mkurugenzi idara ya Misitu Said Juma Ali na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi mazingira ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Sheha mjaja juma wamesema shuhuli hiyo ya Upandaji
Miti inakwenda Sambamba na program ya kuiirejesha Zanzibar kuwa ya kijani na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi lengo lake ni kuihamasisha jamii kupenda, kutunza na kupanda miti.
Vile vile Walisema harakati hizo za kurejesha Zanzibar ya kijani wameamua kila mwaka kupanda miti milioni Tatu mjini na Vijijini na kuanzisha Misitu ya Hifadhi ili kurirhiwa na Vizazi Vijavyo.
Wakizungumza kwa niaba ya Wananchi wenzao walioshiriki katika kazi ya upandaji miti mohamed Ali Sheha na Arafa Hamad Bakari wamesema wamewaomba wananchi wenzao kuendelea kuitunza Misitu kwa kupanda Miti na kuepuka kuharibu mazingira ili malengo yalikusudiwa na Serikali yaweze kufikiwa.
Jumla ya Miti yote iliyopandwa katika Shamba hilo ni elf kumi ambapo miti hiyo ni Mivinje, Mikeshia na MISenna ambayo imepandwa katika eneo lenye Ukubwa wa hekta 4.