28/04/2026
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mhe. Juma Sururu Juma, amesema Programu ya U-Report itawasaidia vijana kupata elimu kuhusu afya ya uzazi pamoja na kinga dhidi ya maambukizi ya VVU, ili waweze kujitambua na kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao.
Ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya Programu ya U-Report yaliyofanyika katika Skuli ya Sekondari Mahonda, Wilaya ya Kaskazini ‘B’, inayotoa elimu kwa vijana wa makundi mbalimbali yakiwemo Mabaraza ya Vijana WA Kaskazini 'B',Madereva wa Bodaboda ,Vijana wa Skaut pamoja na Red Cross.
Amesema mafunzo hayo yatawasaidia vijana hao kujenga uelewa wa kufanya maamuzi bora na kukabiliana na changamoto zinazowakabili, ikiwemo ubakaji na mimba katika umri mdogo.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji pamoja na wafadhili kutoka UNICEF kwa juhudi zao za kuwaelimisha vijana ili kuepukana na vishawishi hatarishi.
Pia amewataka vijana hao kutumia vyema mafunzo hayo kwa kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao na kuchangia ustawi wa vijana katika jamii ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa Programu ya U-Report kutoka Idara ya Maendeleo ya Vijana, Sheila Makungu Mwinyi, amesema mafunzo hayo yanasaidia kuongeza uelewa wa afya ya uzazi, maambukizi ya VVU, magonjwa ya kuambukiza Kuzuia mihemko pamoja na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo.
Ameeleza kuwa vijana wana haki ya kushiriki na kushirikisha katika maamuzi na kueleza changamoto zinazowakabili, huku akibainisha kuwa bado kuna upungufu wa uelewa wa masuala ya afya unaochangia kudhoofisha maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Naye Mkufunzi kutoka Tume ya Ukimwi Zanzibar, Khamis Hassan, amesema elimu ya kujitambua ni muhimu katika kupunguza maambukizi ya magonjwa, ikiwemo VVU, na kuwahimiza vijana kupima afya zao mara kwa mara, hasa kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kuepuka tabia hatarishi na kuwa waaminifu katika mahusiano ili kujikinga na maambukizi.
Aidha, ameeleza kuwa matumizi sahihi ya dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV) husaidia kupunguza virusi mwilini na kuimarisha kinga ya mwili.
Kwa upande wake, Afisa kutoka Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto Wizara ya Afya, Fatma Ussi Yahya, amesema uzazi wa mpango husaidia kupanga familia, kulinda afya ya mama na mtoto, pamoja na kuimarisha ustawi wa familia.
Amewataka vijana kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, akisisitiza kuwa afya ya kijana ni msingi wa ustawi wa taifa.
Mafunzo ya Programu ya U-Report yamefanyika katika wilaya tano za Unguja na nne za Pemba, yakifadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF.