01/09/2026
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame, amewataka wafanyakazi na walinzi wa Hifadhi ya Taifa Jozani Ghuba ya Chwaka kuendelea kulinda na kutunza rasilimali zilizopo katika hifadhi hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Waziri Makame ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi sare za kazi (uniform) kwa wafanyakazi 65 wa Hifadhi ya Taifa ya Jozani, iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema utoaji wa sare hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hususan katika ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za hifadhi hiyo, pamoja na kuwabaini watu wasiohusika wanaoingia katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Amesema Hifadhi ya Msitu wa Jozani ni miongoni mwa maeneo ya hifadhi yanayotambulika kimataifa, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuilinda, kuihifadhi na kuiendeleza ili iendelee kuwa kivutio bora kwa watalii wanaoingia nchini.
"Nawaomba tuendelee kuulinda rasilimali hii ya msitu, kwani kufanya hivyo kutasaidia kuongeza kipato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,” alisema Makame.
Aidha, Waziri Makame ametoa wito kwa wafanyakazi na walinzi wa hifadhi hiyo kuendelea kupatiwa mafunzo ya ulinzi na uhifadhi ili wawe na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha rasilimali za hifadhi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu, Said Juma Ali, amesema sare hizo zimetolewa kwa lengo la kuwatambulisha wafanyakazi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ndani ya hifadhi, pamoja na kuongeza ufanisi katika shughuli za ulinzi na uhifadhi.
Amesema utoaji wa sare hizo ni utaratibu unaofanyika kila baada ya miaka mitatu, ambapo fedha za ununuzi wake hutokana na mapato yanayopatikana katika Hifadhi ya Taifa Jozani.
Amewataka wafanyakazi hao kutumia sare hizo ipasavyo na kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii ili kuhakikisha rasilimali za hifadhi hiyo zinaendelea kulindwa na kunufaisha jamii.
Nae mmoja wa wafanyakazi aliyepokea sare hizo, Mauli Makame Haji, amesema sare hizo zitawasaidia kutambulika kwa urahisi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao katika hifadhi hiyo.
Ameiomba Idara ya Misitu kuendelea kutoa ajira zaidi ili kuongeza idadi ya wafanyakazi na walinzi, hatua ambayo itasaidia kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Jozani.
Jumla ya Shilingi milioni 18.65 zimetumika kununua sare hizo, ambazo zitanufaisha walinzi, watembezaji watalii, pamoja na watumishi wa Usafi.