Mahkama ya Zanzibar

Mahkama ya Zanzibar Contact information, map and directions, contact form, opening hours, services, ratings, photos, videos and announcements from Mahkama ya Zanzibar, Government Organization, BOX NO 160, ZANZIBAR, Zanzibar.

JAJI MKUU WA ZANZIBAR AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA TAASISI YA BASELJaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, leo ...
07/09/2026

JAJI MKUU WA ZANZIBAR AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA TAASISI YA BASEL

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, leo tarehe 7 Septemba 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Taasisi ya Basel, uliofika ofisini kwake kwa ajili ya kumsalimia na kumueleza kuhusu kuanza rasmi kwa kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.

Zoezi hilo linalenga kukusanya maoni yatakayosaidia katika kuandaa mwongozo wa usimamizi wa vielelezo vinavyopokelewa Mahkamani, ili kuhakikisha vielelezo hivyo vinapokelewa, vinahifadhiwa na kusimamiwa kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotumika.

Mwongozo huo unatarajiwa kuweka utaratibu madhubuti wa usimamizi na utunzaji wa vielelezo katika hatua zote za shauri, kuanzia vinapowasilishwa na kupokelewa Mahkamani, kipindi chote cha usikilizaji wa shauri, hadi Mahkama inapotoa amri ya mwisho kuhusu vielelezo hivyo.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa vielelezo Mahkamani, kuongeza uwazi na uwajibikaji, pamoja na kuhakikisha usalama na uadilifu wa vielelezo katika mchakato mzima wa utoaji wa haki.

06/09/2026
Mahkama ya Zanzibar imefanya kikao na wananchi wa Nungwi kwa lengo la kumtambulisha Mkandarasi, PARIK LTD CO., anayeteke...
03/09/2026

Mahkama ya Zanzibar imefanya kikao na wananchi wa Nungwi kwa lengo la kumtambulisha Mkandarasi, PARIK LTD CO., anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Mahkama ya Wilaya ya Nungwi.

Kikao hicho kimefanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja pamoja na Ofisi ya Sheha wa Shehia ya Bandakuu, Nungwi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwashirikisha wananchi na kuwapatia taarifa kuhusu kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi huo.

Katika kikao hicho, wananchi walipata fursa ya kufahamishwa kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa majengo ya Mahkama katika maeneo ya Nungwi na Kinduni, pamoja na kutambulishwa kwa mkandarasi anayehusika na kazi hiyo.

Ujenzi huo ulianza rasmi tarehe 24 Agosti 2026 na unatarajiwa kukamilika tarehe 24 Agosti 2027.

Mradi huu unatekelezwa na Mahkama ya Zanzibar kupitia Mradi wa Maboresho ya Mahkama ya Zanzibar (Zi-JUMP), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (World Bank).
Ujenzi wa majengo hayo ni sehemu ya juhudi za Mahkama ya Zanzibar za kuboresha miundombinu ya utoaji haki, kusogeza huduma za kimahkama karibu na wananchi na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa urahisi, ufanisi na wakati.

ZANZIBAR KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAJAJI WAKUU WA NCHI ZA KUSINI NA MASHARIKI MWA AFRIKA – OKTOBA 2026Jaji Mkuu wa Za...
20/08/2026

ZANZIBAR KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAJAJI WAKUU WA NCHI ZA KUSINI NA MASHARIKI MWA AFRIKA – OKTOBA 2026

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amesema Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), utakaofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 9 Oktoba 2026, katika Hoteli ya Verde, Mtoni, Zanzibar.

Jaji Mkuu ameyasema hayo leo, tarehe 20 Agosti 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mahkama Kuu Tunguu, kwa lengo la kuelezea maandalizi, umuhimu na manufaa ya mkutano huo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Amesema Mahkama ya Zanzibar imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa, unaolenga kuwakutanisha Majaji Wakuu na viongozi wa Mahkama kutoka nchi 17 za Afrika kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazohusu utoaji wa haki na kuweka mikakati ya kuimarisha utawala wa sheria.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na takribani washiriki na waalikwa 150 kutoka Afrika na maeneo mengine duniani, wakiwemo Majaji Wakuu 16 kutoka nchi wanachama wa SEACJF.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa miongoni mwa mada muhimu zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni uongozi wa Mahkama katika kusukuma mageuzi ya kitaasisi, njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), mabadiliko ya kidijitali katika Mahkama, uimarishaji wa usimamizi wa Mahkama, pamoja na matumizi ya Akili Unde (AI) katika utoaji wa haki.

Ameongeza kuwa mada inayohusu mabadiliko ya kidijitali katika Mahkama, ikijumuisha ufunguaji wa mashauri kwa njia ya kielektroniki, usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na mifumo ya usimamizi wa mashauri, itawasilishwa na wenyeji, Mahkama ya Zanzibar.

Akizungumzia manufaa ya mkutano huo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Jaji Mkuu amesema mkutano huo utatoa fursa ya kuongeza ujuzi na kubadilishana uzoefu katika matumizi ya teknolojia katika Mahkama, Akili Unde, usimamizi wa mashauri na njia mbadala za utatuzi wa migogoro.

Aidha, mkutano huo unatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa baina ya Mahkama, kuitangaza Zanzibar kupitia utalii wa mikutano, kuchangia katika ongezeko la shughuli za kiuchumi na mapato ya Serikali, pamoja na kutoa fursa za mafunzo na kujenga uwezo wa Majaji na maofisa wa Mahkama.

Mkutano utafanyika chini ya kaulimbiu:
“Transforming Justice Delivery: Innovation, Efficiency and Court Administration Reform.”
Kaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa ubunifu, ufanisi na mageuzi katika usimamizi wa Mahkama ili kuimarisha utoaji wa haki.

Jaji Mkuu amesema miongoni mwa viongozi wakuu wanaotarajiwa kushiriki katika mkutano huo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi wa mkutano huo.

Pia, Makamu wa Rais wa Botswana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Mhe. Ndaba Nkosinathi Gaolathe, anatarajiwa kuwa miongoni mwa viongozi watakaoshiriki katika mkutano huo.

SEACJF ni jukwaa la kikanda lililoasisiwa mwaka 2003 nchini Afrika Kusini, linalowakutanisha viongozi wa mihimili ya utoaji haki kutoka takribani nchi 17 za Afrika. Jukwaa hilo linalenga kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma, kuboresha usimamizi wa Mahkama, kubadilishana uzoefu na kuendeleza misingi ya sheria na utawala bora.

Address

BOX NO 160, ZANZIBAR
Zanzibar
255

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Mahkama ya Zanzibar posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Shortcuts

Share